Watoto Waliouawa Walikuwa Wanafunzi

Sakata la kuuawa kikatili kwa watoto wawili wa shule ya Msingi Manzese jijini Dar es Salaam, limeingia hatua mpya baada ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo kujitokeza na kuwatetea kuwa hawakuwa na tabia za wizi wala udokozi.

Sakata la kuuawa kikatili kwa watoto wawili wa shule ya Msingi Manzese jijini Dar es Salaam, limeingia hatua mpya baada ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo kujitokeza na kuwatetea kuwa hawakuwa na tabia za wizi wala udokozi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Said, aliiambia Nipashe ofisini kwake kuwa amesikitishwa sana na kitendo cha kuuawa kwa wanafunzi hao kwa kuwa walikuwa hawana tabia ya udokozi.

Marehemu hao ni Emmanuel Malobya (16) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita na Bakari Ramadhani (14) anayesoma darasa la tano, waliuawa Jumamosi iliyopita na wananchi wenye hasira kali wakihusishwa na wizi wa vioo viwili vya pembeni vya gari.

Mwalimu Said alisema kuwa kamwe hawakuwa na tabia za wizi na wala hawakuwahi kutolewa taarifa kama hizo kwa kipindi chote cha uhai wao.

“Juzi baba mlezi wa Emmanuel alinipigia simu kunijulisha jambo hilo, lakini nikawa kama siamini, lakini leo nimesoma katika gazeti la Nipashe nikapata uhakika zaidi,“ alisema Said.

Aliongeza kuwa kwa sasa shule zimefungwa, ila wanafanya utaratibu kama uongozi wa shule kwenda kuwaona wafiwa ila shule itakapofunguliwa mapema mwezi ujao pia wanafunzi watapata nafasi ya kwenda kutoa rambirambi.

Mwalimu huyo aliliomba jeshi la polisi lifanye uchunguzi kwa umakini wa hali ya juu ili kubaini chanzo cha kuuawa kwa wanafunzi hao na watakaobainika wachukuliwe hatua kali.

Aidha, aliishauri jamii kubadilika na kuacha ukatili kama huo na kuongeza kuwa hata kama ingekuwa ni kweli watoto hao wamefanya hivyo, hawakustahili adhabu ya kifo.

Mwalimu huyo alisema kuwa tukio kama hilo ni la kwanza kutokea shuleni hapo ingawa alikiri kuwa kuna wanafunzi wengine wawili wamefariki katika kipindi cha mwaka huu kutokana na maradhi ya kawaida.

Naye mwalimu wa darasa alilokuwa akisoma marehemu Emmanuel, Dainnes Magohe, alisema wanafunzi hao na hasa Emmanuel walikuwa wataratibu na hawakuwa na tabia za wizi wala ya udokozi.

Alisema maendeleo yao darasani yalikuwa mazuri na hata siku ya kufunga shule ambayo ni siku moja kabla ya kukutwa na mauti walikuwa shuleni na wenzao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents