Habari

Watu 2 wauawa kufuatia ghasia kati ya wafuasi wa rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto Kenya

Polisi nchini Kenya wamethibitisha kwamba watu wawili walifariki katika makabiliano ya siku ya Jumapili kati ya wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Bw. Ruto, ambaye alikuwa anahudhuria ibada ya kanisa katika eneo la Murang’a, ngome ya rais Kenyatta iliopo eneo la kati Kenya, alilaani tukio hilo lililowalazimu polise kurusha vitoa machozi ndani ya kanisa kuwatawanya vijana waliokuwa wakishambuliana kwa mawe , kuchoma magurudumu ya magari na kufunga barabara kuu na kusababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Rais Kenyatta – ambaye yuko nchini Ufaransa kwa ziara ya kikazi – na Bw. Ruto wametofautiana vikali katika hatua ambayo imewafanya maafisa wa chama tawala – Jubilee- kupendekeza naibu wa rais kuondolewa kama naibu kiongozi wa chama hicho kilichobuniwa mwaka 2012.

Ruto anapania kumrithi Kenyatta kama rais mwaka 2022 lakini anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wafuasi wa Kenyatta wanaodai kuwa ameanza kufanya kampeni mapema miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

Wawili hao waliingia madarakani wakiahidi kuunganisha taifa na kukomesha migawanyiko ya kisiasa lakini serikali yao imelaumiwa kwa kuzidisha migawanyiko ya kikabila na ufisadi ambao umesababisha nchi kupoteza mamilioni ya dola – ikiwemo dola milioni 7.8 za kununua vifaa vya kukabiliana na Covid 19, ambayo sasa inaasadikiwa huenda zimeibiwa.

Kwa mujibu wa BBC. Uchunguzi wa awali na repoti za Tume ya kukabiliana na ufisadi, Kamati ya bunge la Seneti na ya ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu nchini Kenya zimefichua kuwa wanasiasa na wafanyabishara ambao ni wandani wa mirengo yote miwili ya chama tawala walihusika na ufujaji wa raslimali za umma.

Ubadhirifu huo na wizi unaodaiwa wa fedha za kukabiliana na virusi vya corona ni masuala ibuka yanayoendelea kuzua mjadala mkali nchini humo.

Pande zote mbili zimekuwa zikilaumiana kuhusu ni nani aliyeiba fedha za umma ambazo zilitengwa kukabiliana na janga la Covid-19.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents