Watu wamiminika Shoprite kununua mkate Sh 340

MkateWATU wengi wamekuwa wakimiminika katika maduka makubwa ya Shoprite Dar es Salaam kununua mikate inayouzwa kwa bei nafuu ya Sh 340 wakati sehemu nyingine inauzwa hadi Sh 900


 



Mwandishi wa Habari Leo


 


WATU wengi wamekuwa wakimiminika katika maduka makubwa ya Shoprite Dar es Salaam kununua mikate inayouzwa kwa bei nafuu ya Sh 340 wakati sehemu nyingine inauzwa hadi Sh 900.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, HabariLeo imekuwa ikishuhudia wateja wengi wakimiminika kwenye maduka hayo na kupanga foleni kwenye kaunta ya mikate kujipatia mikate hiyo.

Baadhi ya wateja waliohojiwa katika maduka hayo, walisema wanakimbilia kununua mikate kwenye maduka hayo kwa sababu ni bei nafuu na inakuwa bado ya moto. Maduka hayo hutengeneza mikate yake papo hapo.

“Naipenda mikate hii kwa sababu ni bei nafuu, lakini pia tunaipata ikiwa ya moto, mtaani wakati mwingine wanatuuzia mikate ya juzi,” alisema Juma Kisoki ambaye alikuwa katika duka la eneo la Kamata. Kisoki ni Meneja Masoko wa kampuni ya DCD Dar es Salaam.

Hassan Said ambaye alisema ni mteja wa muda mrefu wa mikate hiyo, alisema kinachomfanya anunue ni ubora wa mikate hiyo kwa sababu inapikwa vizuri na inaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika.

Wakati bei ya mikate katika maduka ya Shoprite ni nafuu, bei katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam ni kubwa maradufu ya ile inayouzwa na maduka ya Shoprite.

Katika maeneo mengi ya jiji mkate unauzwa kati ya Sh 600 na Sh 900 kitu ambacho kimesababisha wengine kuacha kuitumia na badala yake wanatumia maandazi na vitafunwa vingine kwa ajili ya kifungua kinywa.

Katika duka la City Supermarket lililopo Mtaa wa Samora, bei ya mkate ambao ni wa ukubwa sawa na ule wa Shoprite ni Sh 700 na mikate mikubwa Sh 900. Nao wanatengeneza wenyewe papo hapo dukani.

Katika duka la Pamba House Supermarket ambalo lipo Mtaa wa Garden ni Sh 800 kwa mkate mmoja wa ujazo wa kawaida na mikate mikubwa ni Sh 1,100 wakati Shoprite mkate mkubwa ni Sh 550 tu.

Hata hivyo, unafuu wa bei ya mikate kwenye maduka ya Shoprite umezua maswali mengi kutokana na bei ya mikate katika maduka mengine ni zaidi ya mara mbili ya hiyo.

Maswali hayo yanatokana na hisia kwamba huenda wauzaji wengine wa mikate wanawaibia wananchi au kuna tatizo la biashara ambalo linasababisha wauze bei juu.

Juhudi za kumpata Meneja Mkuu, Fredrick Skein wa Shoprite kueleza unafuu wa bei hiyo hazikuzaa matunda, lakini HabariLeo ilizungumza na Meneja Masoko Mathew Kaubo ambaye alisema yeye hana ruhusa ya kuzungumza na waandishi hadi apewe kibali cha kuzungumza.


 


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents