Watuhumiwa wote kasoro mmoja EPA wapewa dhamana

NI mtuhumiwa mmoja tu ambaye amesalia mahabusu kati ya watuhumiwa 20 walioshtakiwa katika kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), baada ya Farijala Hussein kutimiza masharti na kuachiwa huru jana.

NI mtuhumiwa mmoja tu ambaye amesalia mahabusu kati ya watuhumiwa 20 walioshtakiwa katika kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu (BoT) baada ya Farijala Hussein kutimiza masharti na kuachiwa huru jana.

Masharti yaliyokuwa yakimzuia kutoka mahabusu ni pamoja na kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh500 milioni. Kutoka kwake sasa kunamfanya kaimu katibu wa BoT, Imani Mwakosya kusalia pekee mahabusu.

Mwakosya anaendelea kusota rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kutoa fedha taslimu Sh104milioni.

Katika kesi hiyo, Maranda na mwenzake wanadaiwa kuiba zaidi ya Sh2.2 bilioni baada ya kughushi na kuwasilisha hati ya uongo katika Benki ya Biashara na kujipatia kiasi hicho cha fedha toka BoT.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa Septemba 8 mwaka 2005 waliwasilisha hati ya uongo kutoka Kampuni ya B Gracery and Co. Ltd ya Ujerumani na kampuni ya Money baada ya kuonyesha kampuni hizo zilikuwa zimesajiliwa na kwamba wao ndiyo walikuwa wakurugenzi.

Katika hatua nyingine kwa mara nyingine kesi ya wizi wa mabilioni ya fedha EPA inayomkabili mfanyabiashara na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na mwenzake Farijala Hussein, jana haikuweza kusikilizwa.

Kesi hiyo namba 1163, ambayo ilikuwa isikilizwe katika hatua ya awali (Preliminary Hearing-PH) mbele ya Hakimu Anyimilile Mwaseba, jana pia haikuweza kusikilizwa baada ya wakili wa washtakiwa hao, Mark Anthony kushindwa kufika mahakamani na hivyo Hakimu Hezron Mwankenja kuiahirisha.

Hiyo ni mara ya pili kwa Wakili Anthony kushindwa kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kesi hiyo baada juzi pia kushindwa kufika kutokana na kile kilichoelezwa baadaye na Maranda, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, kuwa wakili huyo alikuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.

Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 21 mwakani itakapoendelea tena mahakamani hapo.

Katika hatua nyingine, kesi nyingine namba 1172 inayowakabili ndugu wawili, Jay Somani na Ajay Somani, jana iliahirishwa hadi Januari 13 itakapokuja tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.

 

Source: Mwananchi

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents