Habari

Waumini wafunga siku 3 kumuombea Rais Magufuli aongeze kasi ya bomoabomoa

Waumini wa Kanisa la The River of Healing Ministry lililopo Kibamba jijini Dar es salaam wakiongozwa na Mchungaji John Kyashama wamefunga kutokula na kunywa kwa muda wa siku tatu porini wakimuombea Rais John Magufuli ili mpango wake wa upanuzi wa barabara ya Morogoro ufanyike kwa haraka.

Mchungaji, John Kyashama akiwa mbele ya kanisa la River Healing Ministry of Tanzania lililopigwa X. (Picha na Salim Shao)

Kanisa hilo ni miongoni mwa nyumba 30 za ibada zilizopigwa alama ya X na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa lengo la kubomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.

Mpaka sasa tayari makanisa mengi yametii agizo na kuanza kubomoa yenyewe huku mengine yakihamisha huduma likiwamo Kanisa la Lutherani Kibamba, lakini kwa Kanisa la The River of Healing Ministry lenyewe limeamua kumuombea Rais Magufuli badala ya kuhama.

“Mimi na waumini wangu tumeamua kufunga kula na kunywa kwa siku tatu kuanzia Jumatatu (juzi) katikati ya shamba langu la ekari nne lililopo Chalinze, Lugoba kwani naheshimu sana uamuzi wake, Maombi haya yanalenga zaidi kumuombea Rais ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa haraka, maana katika utawala wake anamuhusisha zaidi Mungu na sisi kama viongozi wa dini hatuna budi kumuombea kama anavyoomba kuombewa”,amesema Mchungaji  Kyashama kwenye mahojiano na gazeti la Mwananchi.

Hata hivyo, Mchungaji huyo amesema hana kinyongo na Rais Magufuli kwa kitendo alichofanya cha kutoa agizo kwa nyumba zilizopo kwenye hifadhi ya barabara zikiwamo za ibada kubomolewa, hivyo wameamua kumuombea ili mipango yake ifanikiwe kwa haraka.

Kuhusu kuhama kwenye kanisa hilo lililopigwa alama X, Mchungaji Kyashama amesema hana mpango wa kuhama kwa sababu hajapata eneo lingine la kuabudia, lakini katika mfungo wanaoufanya Mungu atamuonyesha njia ya kupata eneo litakalotumika kuendeshea ibada.

“Rais ni taasisi kubwa, ninaamini (Mungu) kabla sijavunjiwa jengo langu la ibada Rais atakuwa ameshamfikia na kumpatia eneo jingine kwa hilo sina shaka la kupata eneo lingine,” amesema Mchungaji Kyashama kwenye mahojiano yake na gazeti la mwananchi.

Mchg, Kyashama, ambaye kanisa lake lina waumini zaidi ya 3,000 alisema uongozi wa Rais Magufuli umekuwa wa kipekee na kihistoria, hivyo kazi ya kanisa ni kuwasisitiza wananchi na kuwafundisha kuishi maisha yanayoendana na imani zao ili kulinda na kuhifadhi upendo ndani ya jamii.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents