Habari

Wazanzibari kuishi maisha marefu

RIPOTI ya Matarajio ya Ongezeko la Idadi ya Watu Tanzania (TNP Vol 12) inayotumika kutengeneza mipango ya Serikali iiliyotolewa na Ofisi ta Takwimu ya Taifa (TBS), imeonesha kwamba wananchi wanaoishi Zanzibar wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuishi umri mrefu kuliko wanaoishi Tanzania Bara.



Na Joseph Lugendo


RIPOTI ya Matarajio ya Ongezeko la Idadi ya Watu Tanzania (TNP Vol 12) inayotumika kutengeneza mipango ya Serikali iiliyotolewa na Ofisi ta Takwimu ya Taifa (TBS), imeonesha kwamba wananchi wanaoishi Zanzibar wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuishi umri mrefu kuliko wanaoishi Tanzania Bara.


Ripoti hiyo iliyokamilika mwishoni mwa mwaka jana na kutolewa hivi karibuni, imeonesha kwamba wananchi wa Zanzibar wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuishi umri wa wastani wa miaka 65 ifikapo mwaka 2025.


Umri huo ni mrefu ikilinganishwa na matarajio ya umri wa wastani wa miaka 61 kwa wananchi waishio Tanzania Bara. Mwaka 2025 ni mwaka uliowekwa kwenye mipango ya Serikali kutimiza malengo yatokanayo na Dira ya Taifa.


Ripoti hiyo ambayo haikubainisha sababu za kuwapo kwa tofauti hizo, ilieleza kwamba Watanzania wote kwa ujumla wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuishi umri mrefu ifikapo mwaka 2025 ikilinganishwa na umri wa wastani kwa Watanzania kama ilivyorekodiwa mwaka 2003.


Kwa mujibu wa taarifa iliyokuwapo kwenye ripoti hiyo mwaka 2003, Watanzania waliokuwa wakiishi Tanzania Bara walikuwa na uwezo wa kuishi wastani wa umri wa miaka 52 na waliokuwa wakiishi Zanzibar waliishi wastani wa miaka 57.


Aidha, wanawake wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuishi umri mrefu kuliko wanaume. Ripoti hiyo ilieonesha kwamba wanaume watakuwa na uwezo wa kuishi wastani wa miaka 59 ifikapo mwaka 2025 wakati wanawake watakuwa na uwezo wa kuishi wastani wa miaka 62.


Kuhusu kiwango cha ongezeko la idadi ya watu, ripoti hiyo ilibainisha kwamba kiwango hicho kinatarajiwa kushuka kutoka asilimia 3 ya kiwango cha ongezeko la idadi ya watu kilichokuwapo mwaka 2003 mpaka kiwango cha asilimia 2.5 kwa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025.


Kwa upande wa Zanzibar, kiwango kinatarajiwa kushuka zaidi ya itakavyokuwa Tanzania Bara kutoka asilimia 3 mpaka asilimia 2.


Ripoti hiyo inahusisha kushuka kwa viwango vya ongezeko la idadi ya watu Tanzania Bara na Zanzibar na kupungua kwa idadi ya watoto kwa kila mwanamke wa kitanzania, kunakotarajiwa mwaka 2025.


Takwimu zinaonesha kwamba wastani wa watoto kwa kila mwanamke mmoja wa kitanzania, unatarajiwa kupungua kutoka wastani wa zaidi ya watoto watano kwa mwanamke mmoja ilivyokuwa mwaka 2003 mpaka kufikia wastani wa chini ya watoto wanne kwa kila mwanamke wa kitanzania.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents