Habari

Wazazi wataka uchunguzi kwa vurugu za Mwembesongo

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Mwembesongo, katika Manispaa ya Morogoro, wamedai kuwa hawahusiki katika vurugu zilizotokea za kuwapiga mawe walimu wa shule hiyo, na kuomba kufanyika kwa uchunguzi kuhusu madai hayo.

John Nditi, Morogoro

 

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Mwembesongo, katika Manispaa ya Morogoro, wamedai kuwa hawahusiki katika vurugu zilizotokea za kuwapiga mawe walimu wa shule hiyo, na kuomba kufanyika kwa uchunguzi kuhusu madai hayo.

 

Pamoja na kukanusha madai hayo ya kuhusishwa na kuwafanyia vurugu walimu hao, wamesema kitendo cha walimu hao kuwaadhibu wanafunzi hao hadharani, hakikuwa cha kiungwana.

 

Kauli ya wazazi hao imetolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Mwambungu, katika mkutano wake na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki.

 

Wazazi hao walidai hakuna mzazi aliyediriki kuwafanyia fujo walimu hao na kwamba vitendo hivyo vimefanywa na vijana na kuomba kufanya uchunguzi wa kina juu ya suala hilo.

 

Kwa mujibu wa wazazi hao, vitendo vya kurusha mawe na kutoa lugha ya matusi haikuwa hatua ya kupata suluhu ya tatizo hilo lililosababisha kuvunjika kwa amani katika eneo hilo.

 

Waliuomba uongozi wa shule hiyo kuendeleza ushirikiano baina yao na walimu ili watoto wao wapatiwe elimu. Akizungumza na wazazi hao katika mkutano huo, Mwambungu, aliwataka wazazi hao kufuata taratibu wanapotaka kuulizia masuala ya watoto wao badala ya kuchukua sheria mkononi.

 

Alisema ili kukabiliana na matatizo yanayoweza kujitokeza, upo umuhimu wa kujenga uzio katika shule hiyo ambayo imezungukwa na makazi ya watu. Shule hiyo imezungukwa na michongoma, hali inayowafanya watu wasiowema kupenya na kuingia maeneo ya shule hiyo.

 

Tukio hilo la vurugu katika shule hiyo lilitokea Januari 24, mwaka huu baada ya wanafunzi 200 wanaosoma katika shule hiyo kupewa adhabu ya kuchapwa viboko hadharani na walimu hao. Hatua hiyo, iliwafanya watu wanaodai kuwa wazazi kuamua kufanya vurugu shuleni hapo.

 

Kutokana na vurugu hizo, iliwalazimu Polisi mkoani hapa kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kufika shuleni hapo na kuwatawanya watu. Watu 16 wanashikiliwa wakituhumiwa kwa vurugu hizo.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents