Habari

Waziri aibiwa

Watu watano wametiwa mbaroni mkoani Mbeya kwa tuhuma za kumuibia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Mark Mwandosya.

Na Mwandishi Wa Nipashe



Watu watano wametiwa mbaroni mkoani Mbeya kwa tuhuma za kumuibia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Mark Mwandosya.


Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Bw. Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao walivunja kwa kutumia funguo bandia na kuiba nyumbani kwa Waziri Mwandosya Desemba 25, mwaka jana usiku, katika kijiji cha Lufilyo , Lwangwa Wilaya ya Rungwe.


Kamanda Kova aliongeza kuwa, watu hao waliiba kompyuta tatu aina ya Compaq, mipira mitatu ya miguu, mashuka matatu, vanishi makopo 10, godoro moja na vitu vingine mbalimbali.


Aliongeza kuwa, Machi 3, usiku watu hao kwa kutumia funguo bandia, walivunja kituo cha kulelea watoto yatima kinachomilikiwa na mke wa Waziri Mwandosya, Mama Lucy, na kuiba kipoza joto kimoja.


Alisema thamani ya vitu vyote vilivyoibiwa ni Sh. 6,438,000 ambapo hadi sasa mali iliyokamatwa ina thamani ya Sh. 5,700,000.


Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hezron Dickson (30), Anathael Mapunda (26), Rashidi Yohana (23), Bariki Martini (21) na Rashid Yohana, (23).


“Juhudi za kutafuta kompyuta moja ambayo bado haijapatikana zinaendelea kwani watuhumiwa walikutwa na mali zote zilizoibiwa baada ya polisi kufanya msako mkali dhidi yao katika Wilaya za Rungwe na Kyela,“ alisema Kamanda Kova.


Hali kadhalika, Bw. Kova alisema licha ya kuwakamata watuhumiwa hao, vibaka, wezi na wanyang`anyi 30, pia walitiwa mbaroni katika msako mkali unaoendelea mkoani Mbeya ili kupambana na uhalifu.


Aliongeza kuwa, msako mkali unaendelea ili kuhakikisha wahalifu mbalimbali wanakamatwa na wananchi wa mkoa huo wanaishi kwa usalama zaidi pasipo kubughudhiwa.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents