Habari

Waziri akiri adhabu ya kifo inaiweka pabaya Serikali

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Dk. Mary Nagu amesema sheria ya adhabu ya kifo kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa makusudi inaiweka katika wakati mgumu Serikali na kuchafua sifa ya utawala bora na haki za binadamu.

Juma Mohammed


WAZIRI wa Sheria na Katiba, Dk. Mary Nagu amesema sheria ya adhabu ya kifo kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa makusudi inaiweka katika wakati mgumu Serikali na kuchafua sifa ya utawala bora na haki za binadamu.


Aliliambia HabariLeo jana kwamba sheria hiyo inakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, akiutaja mkataba wa Afrika na ule wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948 kuwa inasisitiza haki ya kuishi. “Sheria ya adhabu ya kifo inatuchafulia sifa yetu ya utawala bora ni adhabu mbaya inayokatisha maisha ya mwanadamu…ni kweli kosa la kuua ni kubwa, lakini thamani yake haiwezi kuwa sawa na ya kuua mtu mwingine.


“Tumeanza kuchukua hatua na Tume ya Kurekebisha Sheria wamefikia pazuri, kwanza tutatoa elimu na mijadala ya wananchi,” alisema. Alisema sheria hiyo inafanyiwa kazi na Serikali kwa lengo la kufutwa na kutunga sheria mbadala baada ya mchakato wa utoaji elimu na kupata maoni ya wananchi kukamilika, kwani kumekuwa na maoni tofauti juu ya sheria hiyo.


Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Robert Kisanga alisema sheria ya adhabu ya kifo inakwenda kinyume na katiba na kuifanya Tume yake kuwa katika mazingira magumu ya utekelezaji wa shughuli zake kwa wananchi.


Akizungumza na HabariLeo, Jaji Kisanga alisema; “Sisi tunawekwa katika hali ngumu kwa sheria hii…tunaomba juhudi zifanywe kuishawishi Serikali kuifuta kwa sababu inakiuka haki za binadamu kabisa.” Alisema kwa kuwa Tume yake ndiyo yenye kuhusika na masuala ya haki za binadamu na utawala bora, jamii imekuwa ikipata taswira tofauti na kuwapo kwa sheria ya adhabu ya kifo hapa nchini.


Jaji Kisanga alisema kwamba mbali ya sheria hiyo kukiuka katiba, lakini pia ni mbaya na ambayo haisaidii kuleta maelewano miongoni mwa jamii, kwa kuwa adhabu ya kifo inaongeza chuki na majonzi kwa wananchi.


“Katika nafsi yangu adhabu ya kifo naichukia na nitaishawishi Serikali kuifuta sheria yenye kutoa hukumu ya kifo… na pia elimu itolewe kuelezea unyama wa adhabu ya kifo ana madhara yake,” alisisitiza.


Alisema kwamba kunahitajika mjadala wa kitaifa kujadili sheria ya adhabu ya kifo na madhara yake kwa jamii, kwa vile sheria hiyo imekuwa ikipigiwe kelele na mashirika na watetezi wengi wa haki za binadamu. Nacho Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, kimewasilisha mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria ya adhabu ya kifo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania baada ya kuombwa na Tume kama mdau kutoa maoni yao.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents