HabariUncategorized

Lugola atoa agizo kali kwa Ma-RC, DC na Polisi, ataka viongozi wa upinzani wanaomtukana Rais wakamatwe

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewaagiza makamanda wa polisi nchini washirikiane na wakuu wa mikoa na wilaya kuchunguza na kuwakamata wapinzani wanaomtukana rais pamoja na Serikali kupitia vikao vyao vya ndani vya siasa.

Related image
Waziri Lugola

Akizungumza na wananchi wa mjini Kilosa jana katika mkutano wa hadhara,  Lugola  alisema ana taarifa kuna baadhi ya wapinzani ambao wanafanya vikao vyao vya ndani huku wakitukana, kubeza pamoja na kuwachonganisha wananchi na Serikali yao ambayo inaongozwa na Rais Dk. John Magufuli.  

“Mimi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sitakubaliana na kiongozi wa chama chochote kuvunja agizo tulilolitoa nchi nzima kwa kutokuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ya siasa na pia kupitia mikutano ya ndani ambayo inafanyika, ambapo baadhi ya wanasiasa wahuni wanamtukana rais ambaye ndiye kiongozi mkuu wa nchi, mimi sitakubaliana na hilo,” alisema Lugola.

Aliwataka wapinzani kuwa wasikivu kwa kufuata sheria za nchi na pia kutambua kuwa rais wa nchi hii ambaye kipenzi cha wananchi anapewa heshima yake kwa kuiletea maendeleo nchi.

Lugola alisema Rais Magufuli ni kiongozi ambaye kwa muda mfupi ameiletea mabadiliko makubwa nchi na pia mipango mikubwa ya maendeleo inakuja katika uongozi wake.

Lugola alifanya mikutano miwili ya hadhara wilayani Kilosa, ambapo mkutano mmoja ulifanyika mjini Kilosa na mwingine ulifanyika Tarafa ya Kimamba wilayani humo, ambapo alizungumza na wananchi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo kupitia kutoa nafasi kwa wananchi kutoa kero zao.

Chanzo: http://mtanzania.co.tz/lugola-aagiza-kukatwa-wapinzani-wanaomtusi-rais/

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents