Habari

Waziri Mkuu aitaka Bodi ijayo ya tumbaku kujipanga

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema tumbaku ni uchumi na ameitaka Bodi ya Tumbaku itakayoundwa ijipange kumlinda mkulima.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.

Alisema wajumbe wa bodi hiyo walishatajwa lakini kwa sasa hivi wanasubiri uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo. Hata hivyo, Waziri alimwelekeza Katibu Mkuu wa Kilimo awaite wajumbe wa bodi hiyo wakutane na kumchagua Makamu Mwenyekiti wa muda ili waanze kazi ya kukutana na WETCU zao.

“Kwa sababu bodi ni ya nchi nzima, ni vema wakakutana na WETCU zao na AMCOS zao ili waanze kukusanya taarifa ya tumbaku kutoka Chunya, Namtumbo, Serengeti na mahali mengine ili wapeleke message hii ya msimu ujao,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema ili kuongeza ufanisi kwenye zao hilo, itabidi baadhi ya majukumu ya bodi yapunguzwe ikiwemo kazi ya utoaji vibali vya kusafirisha na kununua tumbaku. “Hivi kama kibali cha kuuza tumbaku ya Namtumbo kinatolewa na Bodi ambayo makao makuu yake yako Tabora, sasa utawezaje kufuatilia kutoka Tabora? Ka nini kazi hiyo isifanywe na chama kikuu cha ushirika kilichopo huo?” alihoji Waziri Mkuu.

Alionya kwamba endapo bodi itaachiwa iingie kila mahali, haitaweza kulaumiwa pindi jambo likiharibika. “Ninyi kazi yenu kubwa iwe ni usimamizi kuanzia kwenye WETCU na AMCOS zake. Simamieni masoko, hakikisheni wanaokuja kununua wako tayari kufuata mfumo uliowekwa na Serikali,” alisema.

Waziri Mkuu alisema bodi ijayo inalo jukumu pia la kushirikiana na vyuo vya utafiti ili kuhakikisha kuwa tafiti zinafanyika na kupata mbegu bora zenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents