Habari

Waziri Mkuu ampa miezi miwili Mkurugenzi wa Halmashauri Songwe

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempa miezi miwili kuanzia leo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe, Elias Nawera abadili mwenendo wake kiutendaji na ashirikiane vizuri na Mkuu wa wilaya hiyo Samwel Jeremiah.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Alhamisi hii, wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Songwe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.

Amesema watumishi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yaweze kufikiwa. Pia waheshimiane sehemu za kazi na kila mtu azingatie mipaka ya madaraka yake.

“Mkurugenzi hapa hamsikilizi Mkuu wa wilaya anaondoka kituo cha kazi bila ya kuaga na amewagawa wakuu wa Idara. Namtaka afanye mabadiliko ya utendaji wake ndani ya miezi miwili na Mkuu wa Mkoa fuatilia jambo hili,” alisisitiza Waziri Majaliwa.

Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote wasimamie utendaji wa wakurugenzi wa Halmashauri kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.”Serikali hii si ya mchezo. Serikali hii inahitaji watumishi waadilifu wa kuwatumikia Watanzania.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bibi Chiku Galawa amesema wamejipanga kuhakikisha changamoto zote zinazoukabili mkoa zinaboreshwa pamoja na kufikia malengo ifikapo 2020.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents