Habari

Waziri Mkuu apangiwe siku kujibu hoja – Wabunge

Waziri MkuuBaadhi ya wabunge wamependekeza Waziri Mkuu apangiwe siku maalum za kujibu maswali yao bungeni badala ya utaratibu wa sasa wa kuwaachia Naibu Mawaziri.

Na Beatrice Bandawe, Dodoma



Baadhi ya wabunge wamependekeza Waziri Mkuu apangiwe siku maalum za kujibu maswali yao bungeni badala ya utaratibu wa sasa wa kuwaachia Naibu Mawaziri.


Pendekezo hilo lilitolewa jana wakati Kamati mbalimbali za Bunge zikiwasilisha� taarifa za safari za kujifunza nje ya nchi.


Akiwasilisha taarifa ya wabunge waliotembelea Bunge la Uingereza, Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alisema wabunge walijifunza kuwa katika bunge la Uingereza, hutengwa siku maalum ya Waziri Mkuu kujibu maswali ya wabunge, bungeni.


Baadhi ya wabunge waliochangia pendekezo hilo, walisema utaratibu huo unasaidia kupima uwezo wa serikali.


Wabunge waliopendekeza hoja ya Waziri Mkuu, kupewa siku maalumu angalau mara moja kwa wiki kujibu maswali bungeni ni Bw. Benedict Losurutia (Kiteto, CCM),�Bw. Chacha Wangwe (Tarime, CHADEMA), Bi. Amina Chifupa (Viti Maalum, CCM), na Bw. Christopher Ole-Sendeka (Simanjiro, CCM).


Akichangia hoja hiyo, Bi. Chifupa alisema, ingekuwa vizuri kama Waziri Mkuu angetengewa siku moja maalumu, mara moja au mara mbili kwa wiki ili kujibu maswali ya wabunge.


Bw. Ole-Sendeka, alipendekeza kuwa badala ya kuwaachia Manaibu Mawaziri kujibu maswali, mawaziri ndio wawe wanajibu pamoja na Waziri Mkuu.


Hata hivyo, akichangia hoja mbalimbali, Naibu Spika, Bi. Anne Makinda, alisema baadhi ya wabunge huuliza maswali marefu, kitendo kinachosababisha baadhi ya maswali kutojibiwa kutokana na kukosa muda wa kutosha.


Aidha, akipokea mawazo mbalimbali ya wabunge katika taarifa, Dk. Mzindakaya, alipendekeza habari za Bunge zinazoandikwa na waandishi wa habari, zichujwe kwanza na Bunge kabla ya kutolewa kwenye vyombo vyao.


Alisema Bunge la Uingereza lina ushirikiano na vyombo vya habari tofauti na Tanzania ambako waandishi wamejenga mawasiliano mabaya.


Alisema vyombo vya habari vimekuwa vikichonganisha wabunge na wananchi wao.


Katika taarifa yake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (Mlalo-CCM), alisema katika Bunge la Canada, maswali ya wabunge bungeni hutolewa papo kwa papo badala ya utaratibu wa kuyaandaa kwanza na baadaye kujibiwa.


Akiwasilisha taarifa ya wabunge katika Bunge la Ghana, Bw. Phares Kabuye (Biharamulo Magharibi, TLP), alisema walichojifunza katika Bunge hilo ni kuwa mawaziri wenyewe ndio wanaojibu maswali badala ya manaibu.


Kwa upande wake, kiongozi wa msafara wa wabunge katika Bunge la Singapore, Bw. Omar Kwaangw� (Babati Mjini, CCM), alisema walichojifunza huko ni kuwa mbunge anawezeshwa kuajiri watalaam kumsaidia katika shughuli zake.


Aidha, kiongozi wa safari katika Bunge la Australia na Uingereza, Bw. John Cheyo (Bariadi Mashariki, UDP), alisema walichojifunza ni kuwa uwekezaji kwenye Bunge ni mkubwa.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents