Habari

Waziri Mkuu apiga marufuku viongozi wa serikali kujihusisha na biashara hii

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Serikali wasiokuwa na mashamba ya mikorosho kutojihusisha na biashara ya uuzaji wa zao hilo.

Waziri Mkuu ametoa agizo Jumapili hii, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika mkoani Tanga.

“Kama huna shamba, huwezi kuwa na korosho, unauza umepata wapi. Jukumu lenu ni kufuatilia, kukemea na kuchukua hatua stahiki penye udhaifu na si vinginevyo.”

Amesema kama viongozi hao wanahitaji kuuza korosho watumie muda huu ambao Serikali inahamasisha watu wafungue mashamba mapya nao watumie fursa hiyo na kulima.

Amesema ni vema kila mdau akahahakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo kama ni mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo na mnunuzi azingatie taratibu zilizopo.

Waziri Mkuu amesema Bodi ya Korosho inatakiwa kuhakikisha inaimarisha zao hilo na kuishauri vizuri Serikali kuhusu namna bora ya kuliendeleza.

Amesema Serikali inaamini kuwa iwapo kila mdau wa zao la korosho atatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuliendeleza zao hilo kila upande utanufaika kikamilifu.

Hivyo, ni vizuri kila mdau ajitathmini kama anatimiza wajibu wake kikamilifu, huku akiwaagiza viongozi wa Ushirika waendeshe Ushirika kwa uadilifu mkubwa.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitakuwa tayari kusikia mkulima yeyote akilalamika kuhusu malipo iwe kwa kupunjwa, kuchelewa ama kutolipwa.

Amesema katika msimu huu wa biashara ya korosho Serikali haitarajii kusikia mambo ambayo yalikwaza ufanisi katika misimu iliyopita kama wakulima kukatwa unyaufu kwa namna yoyote.

“Sheria ya unyaufu ni miezi sita kutoka korosho inapoanza kuvunwa hadi kuuzwa na korosho haifiki miezi sita, hivyo wakulima hawahusiki unyaufu kwa namna yoyote ile na tusisikie tena.”

Amesema hali hiyo ikitokea hawatasita kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika. “Nawaagiza viongozi wa ngazi zote kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa jambo hili.”

Pia amepiga marufuku Bodi ya Maghala kutoza ushuru wa kuhifadhi mazao kwani hilo si jukumu lao bali ni la mpangaji wa ghala na wao washughulikie utoaji wa leseni tu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa maghala ya kuhifadhia korosho kutowazuia Viongozi wa Serikali kuyakagua kabla na wakati wa biashara.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents