Habari

Waziri Mkuu aridhishwa na ujenzi wa Gati

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la mradi wa ujenzi wa gati kwenye Manispaa ya Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wake.

Waziri Mkuu alitembelea mradi huo Ijumaa hii, wakati alipotembelea eneo hilo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati hilo, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo, hivyo ujenzi wa gati hilo uende kwa kasi huku ukizingatia matakwa ya kiufundi na ubora wa hali ya juu.

“Jengeni sehemu ya kupumzikia abiria katika pande zote mbili, upande wa Lindi na wa Kitunda. Mbali na abiria kupata eneo la kupumzikia pia itarahisisha hata ukataji wa tiketi jambo litakawarahisishia ukusanyaji wa mapato.”

Pia Waziri Mkuu aliwaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kwamba ahadi zote zilizoahidiwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zitatekelezwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kuyafanyia maboresho maeneo ya pwani na kuwa ya kisasa kwa kuondoa majengo yote chakavu ili wananchi waweze kuyatumia kwa ajili ya kupumzikia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents