Habari

Waziri Mkuu atoa miezi 3 kwa waliojenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao kuanzia umbali wa mita 50.

Pia ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika wazibomoe.

Agizo hilo amelitoa Ijumaa hii, alipotembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, ambacho kinajengwa na Serikali ya Tanzania na kitagharimu sh. bilioni 12.

“Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha Serikali mapato,” alisema Waziri Majaliwa.

Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari.

“Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia.”

Awali Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Bw. Field Simwinga ambaye alisema wamekubaliana na utekelezaji wa agizo hilo kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents