Habari

Waziri Mkuu awataka wauguzi kufanya kazi kwa weledi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wauguzi nchini kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na kufuata maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.


PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatano hii, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.

“Nanyi Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa,”alisema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Majaliwa alipiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wakiwemo wauguzi bila ya kufuata taratibu.

“Naagiza viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma, Mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya Wanataaluma wa Afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati mbalimbali iliyopangwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.

Hata hivyo Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania wote zinaimarika ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya kuinua uchumi na kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamis Kigwangalla awali alisema baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa Sekta ya Afya bila ya kufuata taratibu, jambo ambalo si sahihi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents