Habari

Waziri Mkuu kuwasilisha bajeti ya ofisi yake Alhamisi hii

Moto wa Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti unazidi kupamba moto, na leo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atawasilisha bungeni bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Waziri Mkuu atawasilisha bungeni hotuba yake hiyo mara tu baada ya kukamilika kwa Kipindi cha Maswali na Majibu. Baada ya kuwasilisha bajeti yake, wabunge watapata nafasi ya kujadili hoja zitazowasilishwa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Mjadala juu ya hotuba hiyo utaendelea hadi Aprili 13, mwaka huu, ikiwa ni muda wa siku 4 ukiondoa siku za mapumziko zitakazotokana na Siku ya Kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, Aprili 7 na mapumziko wa mwisho wa juma.

Wakizungumza na gazeti la Habarileo, baadhi ya wabunge walisema wanatarajia Waziri Mkuu kuwasilisha hotuba itakayokuwa na majibu ya masuala mbalimbali yanayoitikisa nchi hivi sasa.

“Tunaamini itajibu masuala mbalimbali hasa yale ya kijamii kuhusu kilimo, maji, afya, miundombinu, lakini pia kuhusu maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa, Venance Mwamoto (CCM).

Naye Mbunge wa Jimbo la Songwe mkoani Songwe, Philipo Mulugo (CCM) akizungumzia hotuba hiyo alisema; “ Nadhani itakuwa ni hotuba yenye msisimko mkubwa kwani Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa shughuli za serikali bungeni.”

Mulugo alisema pamoja na mambo yanayotokana na matukio, ana imani kubwa hotuba ya Waziri Mkuu itakuwa na majibu ya mwendelezo wa utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyoahidiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents