Moto Hauzimwi
Shinda na SIM Account

Waziri Mpina amsimamisha kazi mtumishi kwa kushiriki kutorosha Kilo 2500 za samaki

Serikali kupitia, Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  imemsimamisha kazi  Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera,  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2500 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/=.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana  Budeba kumsimamisha  kazi mara moja Afisa huyo kwa tuhuma hizo zinazo mkabili.

Akizungumza katika ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina  alisema  mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00  asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.

“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na  barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja.” Alisisitiza Mpina

Aidha, Waziri alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo,  na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.

Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa  walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50, msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.

Waziri Mpina  alisema samaki hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.

Alisema  kazi hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa, uchunguzi wa awali ilibaini kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo wilayani Muleba.

Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na  kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama na watuhumiwa wawili kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo.

Kukamatwa  kwa uduvi kilo 5000 ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi 100,000/=,kukamatwa  kwa mafurushi 6 ya Samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 katika kituo cha Basi cha Bukoba zilizokuwa zikitoka mkoani Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao kutaifishwa.

Katika tukio jingine jumla ya kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki yamekamatwa kwenye doria mpakani Mtukula na mtuhumiwa  amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.

Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia  katika  uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Wakichangia kwa nyakati tofauti watumishi wa kituo hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina kuangalia namna ya kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.

Leave a comment

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW