Habari

Waziri Mwakyembe atoa shukrani kwa Watanzania

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe ameshukuru viongozi mbalimbali wa Kiserikali na pamoja na wananchi kwa ujumla na viongozi wa dini na waandishi wa habari kwa ushirikiano alioupata wakati wa Msiba wa Marehemu Mke wake Linah George Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe ametoa shukrani hizo leo wakati akizungumza nyumbani kwake, kunduchi jijini Dar es salaam.

Taarifa kamili ya shukrani:

Napenda kutumia fursa hii kwanza kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka zake na pili kutoa shukrani zangu za dhati kwa Watanzania wote kwa upendo na ushirikiano mkubwa mlionipa mimi na familia yangu katika kuomboleza kifo cha mke wangu mpendwa Bi.Linah Widmel-George Mwakyembe na baadaye katika mazishi
yake wilayani Kyela.

Familia inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kwa mchango wao mkubwa katika kumuuguza marehemu wakati wa uhai wake.

Aidha, familia inawashukuru viongozi hao waandamizi wa nchi pamoja na Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Naibu Spika, Mhe. Tulia Ackson Mwansasu, wake wa viongozi, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, viongozi wetu wa nchi wastaafu, Wabunge, Majaji, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Maaskofu wa Kanisa la Kiluteri, Makanisa ya Moravian na makanisa ya
kiroho (Mito ya Baraka, Living Water, Evangelical Brotherhood nk) kwa ushirikiano wao katika maombolezi na mazishi ya marehemu.

Wana-familia tutakumbuka daima moyo adhimu wa upendo na ushirikiano tulioupata toka kwa Katibu wa Bunge na maafisa wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na timu yake mzima ya Wizara, Makatibu Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, watendaji wakuu wa taasisi, asasi na kampuni mbalimbali, na wananchi wote kwa ujumla katika kipindi hicho kigumu.

Pia napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru Wana-Kyela wote kwa uvumilivu waliouonesha kipindi chote cha kumuuguza marehemu na ushirikiano wao wa dhatikatika mazishi yake.

Mwisho lakini si kwa umuhimu, nawashukuru sana madaktari na wauguzi waliomhudumia marehemu kwa kujituma, kwa weledi na ustahimilivu wao ili kuokoa maisha yake lakini Mungu akampenda zaidi. Vilevile wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi na watangazaji kwa kukesha nasi kipindi chote cha msiba Dar .

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents