Burudani

Waziri Mwigulu awataka walimu kutosita kutumia fimbo mashuleni

Waziri wa Mambo ya ndani, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka walimu nchini kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwa kuwafundisha maadili mema na pale inapobidi matumizi ya fimbo yatumike wasisite kufanya hivyo.

Akizungumza katika harambee ya ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari Lulumba Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Dkt. Nchemba alisema walimu wanatumia fimbo kunyoosha nidhamu za wanafunzi ili kutengeneza hatma ya nchi.

“Kuna wakati walimu wananyoosha nidhamu za wanafunzi lakini ninyi hamuoni hii na kulalamika tu, kinachofanyika ni kwa manufaa yetu…niwaombe kwenye kutumia mifano tumieni mifano na kwenye kutumia fimbo fanyeni hivyo ili kutengeneza taswira ya nchi yetu,” alisema Dkt. Mwigulu.

Alisisitiza kuwa ni lazima kuendelea kulinda hadhi za walimu kwa kuwapatia miundombinu bora ya ofisi na vyumba vya madarasa.

“Naunga mkono ujenzi huu wa mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu hivyo nachangia mifuko 200 ya saruji nawaahidi pia kutoa Sh milioni sita,” alisema.

Katika harambee hiyo, saruji iliyokusanywa ni mifuko 209, ahadi ya fedha ni 8,486,000, ahadi ya mifuko ya saruji 572, Gypsum 50 na nondo tani moja jumla ya ahadi na fedha taslimu ni 19,494,300.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents