Habari

Waziri Nchemba atoa agizo kwa wananchi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza wananchi kushirikiana na serikali katika ujenzi wa vituo vya polisi kwa kuwa suala la ulinzi ni ajenda ya kila Mtanzania na linapaswa kupewa kipaumbele.

Akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mwigulu alisema kuwa mkakati wa halmashauri hiyo kujenga kituo cha kisasa cha polisi ni cha kupongezwa kwani wanalenga kukomesha uhalifu wa aina zote.

Aidha Mwigulu alisema maeneo mengi nchini yanahitajika vituo vya polisi na kwamba serikali pekee haiwezi kujenga vituo hivyo kwa siku moja badala yake wananchi na wadau wanaweza kusaidia ujenzi huo.

’’Ujenzi huu wa kituo cha polisi utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwani bado kunahitajika vituo vingi zaidi hapa nchini na serikali haiwezi kujenga kwa siku moja. Wizara itaangalia namna ya kuwasaidia kwenye ujenzi huu name nitatoa nondo 500, mifuko ya saruji 500 na fedha za mafundi,’’ alisema Dk Mwigulu.

Hata hivyo amelitaka jeshi la polisi kutafuta namna ya kurekebisha wahalifu wanaokamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo uzururaji ili kupunguza mrundikano katika mahabusu.

Alisema kuwa ipo haja ya kuangalia utaratibu wa urekebishaji wa watuhumiwa wa makosa hayo ili wasiweze kupata nafasi ya kuzungumzia masuala ya uhalifu na watuhumiwa waliozoea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Happiness Seneda alisema kuwa wilaya hiyo inavituo vitatu pekee vya polisi ambavyo havitoshi na mazingira yake hayaridhishi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents