Habari

Waziri Nchemba atoa shavu la ajira kwa vijana sita

Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza vijana sita ambao wanafanyakazi ya kujitolea katika mradi wa kiwanda wa cha sukari cha Mbigiri wilayani kilosa mkoa wa Morogoro majina yao yapelekwe wizarani wapate ajira ya kudumu.

Hatua hiyo imefikia baada ya waziri Mwigulu kufika kiwandani hapo na kupata taarifa ya kinachoendelea kiwandani hapo na kuambiwa kuwa kuna vijana sita wenye taaluma mbalimbali ambao wanajitolea na wamefanya kazi kubwa ya ujenzi wa kiwanda hicho na wengine kuchora ramani ya baadhi ya majengo yenye umbo la ndege aina boeing.

“Msimamizi wa mradi chukua majina ya hawa vijana yalete wizarani, tutayapeleka utumishi ili hawa vijana wazalendo wawe ndio wafanyakazi wa kwanza wa kiwanda hichi kwani kujitolea kwa miezi sita bila kulipwa tena kijijini ni uzalendo wa hali ya juu na wanaipenda nchi yao,” alisema Mwigulu.

Waziri Nchemba amepongeza hatua iliyofikiwa mpaka sasa katika mradi huo kwani sehemu kubwa ya miwa iliyopo shambani imekua mikubwa na kwa taarifa alizopewa ifikapo mwezi wa nane mwaka huu wataanza kuvuna miwa na sukari ya kwanza kutoka kiwandani hapo itatoka oktoba mwaka huu.

Naye Msimamizi wa mradi wa kiwanda cha sukari Mbigiri Eng Robert Kabudi amesema kwasasa wanaingia makubaliano na kampuni moja kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha sukari na kuleta mitambo ambapo kwa makadilio ifikapo mwezi wanane kiwanda kitakua kimekamilika na kuanza uzalishaji wa sukari.

“Mvua kutokunyesha ya kutosha imekua changamoto kwetu hasa katika kupanda miwa mingi zaidi kwa ekari zilizobaki lakini tunaendelea kuchimba visima vingi zaidi kwa ajili ya umwagiliaji shambani na tunaendela vizuri mpaka sasa kama unavyojionea na ifikapo mwezi wa nane mwaka huu tutaanza kuvuna awamu ya kwanzu mheshimiwa” alisema

Eng Robert ameongeza kuwa mpaka sasa wameongezewa ekari 200 na wilaya ya kilosa ambapo wanampango wa kujenga shule, kituo cha polisi na malls na mabenki ilikufanya kijiji cha mbigiri kuwa cha kisasa kama kilombero na sehemu zingine za viwanda ili wafanyakazi baadae wasifate huduma mbali.

Kiwanda cha sukari cha mbigiri ni cha ubia kati ya jeshi la magereza nchini na mifuko ya kijamii ya NSSF NA PPF na kinatarajiwa kuanza kutumika mwezi october mwaka huu na uzalishaji wake utakua ni zaidi ya tani 30000 za sukari kwa mwaka.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents