Habari

Waziri Ummy aagiza vyakula vya kwenye maharusi vichunguzwe

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Wizara ya Afya, Kitengo cha Afya ya Mazingira, kuangalia ni Mamlaka ipi inajukumu la kutazama vyakula vinavyoliwa kwenye maharusi, ili kulinda afya za walaji.

Waziri wa afya, Ummy Mwalimu (kulia) akipata maelezo juu ya sukari zinazopimwa ubora wake kutoka kwa Mkuu wa Maabara wa TFDA Kanda ya Ziwa Salum Kindoli alipotembelea kukagua shughuli za ujenzi wa jengo la Mamlaka hiyo jijini Mwanza.

Waziri Ummy Mwalimu ametoa maagizo hayo, alipotembelea kuangalia ujenzi wa jengo la TFDA ambalo linajengwa Jijini Mwanza ili kusogeza huduma kwa wananchi wa mkoa huo.

Waziri Ummy amesema kuwa vyakula hivyo vimekuwa vikisafirishwa umbali mrefu bila kujua vinaandaliwa katika mazingira yapi na kubebwa kwa usalama wa hali gani ili kulinda afya za walaji.

“Hatutaki kuharibu biashara za wajasiriamali wa vyakula lakini tunahitaji kufahamu mazingira ya uandaaji wa vyakula hivyo pamoja na vifungashio wanavyotumia, kuna familia imewahi kulazwa Muhimbili mara baada ya kula chakula harusini na hivyo nawapa agizo hilo mkalifanyie kazi”, amesema Waziri Ummy.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa TFDA ina wajibu wa kusimamia Tanzania isiwe jalala la bidhaa zisizo na ubora kwa watanzania hivyo wanatakiwa kuweka afya ya wananchi mbele kuliko manufaa binafsi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents