Habari

Waziri Ummy atoa agizo kwa maafisa maendeleo ya jamii

Serikali kupitiaWaziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy  Mwalimu  imewataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kurejesha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika kazi za maendeleo ili kutoa mchango katika kufikia Tanzania ya Viwanda na yenye uchumi wa kati.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akisisitiza maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kuelekea uchumi wa Viwanda wakati akifungua Mkutano wa wataalam wa Sekta ya Mandeleo ya Jamii unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini Dodoma.

Kauli hii ya Waziri Ummy imetolewa Mjini Dodoma na  wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii unafoanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini humo.

Mhe. Ummy  amesema kuwa kupitia Mkutano huo Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wanatakiwa  kutoa  mapendekezo kuhusu mbinu bora zitakazosaidia kurudisha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika maendeleo na hivyo kusaidia kufikia uchumi  wa kati na wa viwanda.

Aidha Waziri Ummy  amefafanua kuwa wataalam wa maendeleo ya jamii ndiyo wenye jukumu la kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya kisekta hususan kilimo, afya, elimu, na miundo mbinu na kadhalika.

“Wataalam wa  Maendeleo ya Jamii watumie fursa hii kujitathmini ili kupata majibu ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kuamsha ari ya wananchi kushiriki kwenye uzalishaji na kutokomeza ukatili wa jinsia ambao unapunguza kasi ya kufikia uchumi wa kati na maendeleo jumuishi” alisema Mhe. Ummy.

Waziri Ummy ameeleza kuwa Kaulimbiu ya Mkutano wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa Mwaka 2017  ambayo ni  “Amsha Ari ya Ushiriki wa Wananchi Kufikia Uchumi wa Viwanda” inatafsiri azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na Tanzania ya Viwanda ili kufikia uchumi wa kati.

Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga amesema kuwa katika awamu ya sasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana wajibu wa kuelimisha na kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi za uzalishaji kwa bidii kwa kuzalisha mali ghafi zinazohitajika na viwanda na kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo na vya kati.

Bibi Sihaba Nkinga amefafanua kuwa malengo ya Mkutano huo umezingatia  tathmini ya mchango wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kuamsha ari na hamasa ya wananchi kushiriki na kuchangia maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wa Sekta na Idara nyingine katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amewaasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau  kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitoa katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo katika maeneo yao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents