Habari

Waziri wa Ulinzi Tanzania akutwa amevunjika mbavu

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Profesa Juma Kapuya ambaye alinusurika katika ajali mbaya ya gari iliyoua watu watatu na kujeruhi wengine wanne, wilayani Urambo, Tabora amevunjika mbavu.

Na Tausi Mbowe


WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Profesa Juma Kapuya ambaye alinusurika katika ajali mbaya ya gari iliyoua watu watatu na kujeruhi wengine wanne, wilayani Urambo, Tabora amevunjika mbavu.


Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Jumaa Almasi alisema jana kuwa uchunguzi umeonyesha kuwa Waziri Kapuya, amevunjika mbavu moja ya upande wa kulia na kupata majeraha sehemu mbalimbali ikiwamo paji la uso baada ya kukatwa na vioo.


Almasi alisema majeruhi wengine wawili akiwamo Msaidizi wa Waziri huyo, Luteni Kanali Leopald Kalima (50), aliyevunjika mfupa wa bega na Shigela Mabula (36), aliyeumia kidole walitibiwa na kuruhusiwa, huku Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Urambo akiendelea kupata matibabu hospitalini hapo katika wodi ya Sewahaji namba 17.


Akizungumza kwa taabu, Waziri Kapuya alisema bado anasikia maumivu makali sehumu za kifua na tumboni na hadi jana alishindwa kujisogeza hivyo kumlazimu kusaidiwa kusogezwa na kugeuzwa.


Profesa Kapuya alinusurika katika ajali mbaya ya gari iliyotokea mapema wiki hii katika kijiji cha Usindi wilayani Urambo mkoani Tabora wakati akitoka katika ziara ya kutembelea wakazi wa jimbo lake.


Kapuya amelazwa wodi maalumu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), baada ya kuhamishiwa hospitalini hapo juzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora ambako alikimbizwa baada ya kupata ajali hiyo.


Kapuya alisafirishwa kutoka mkoani humo kwa ndege ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar Salaam na kupelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.


Wakati huo huo; viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Shein, jana walifika hospitalini hapo kumjulia hali Waziri Kapuya.


Wengine ni Naibu Waziri wake Omari Yussuf Mzee, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Dk Batilda Burian, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Ritta Mlaki, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu.


Wengine ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Abdulrahman Shimbo, Mkuu wa Utumishi wa JWTZ, Brigedia Jenerali Samwel Ndomba, Mbunge wa Mkuranga Adam Malima, Mbunge wa Temeke Abass Mtemvu na maafisa mbalimbali wa JWTZ.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents