Habari

Wazungu ‘waroga’ hoteli ya mshindani wao

VITENDO vya kishirikina vimeanza kuigubika sekta ya utalii visiwani humu kufuatia tukio la hivi karibuni, ambapo mwekezaji mmoja anayemiliki hoteli ya kitalii iliyopo katika eneo la Mji Mkongwe, kufanyiwa vitendo vya kishirikina ndani ya sebule ya hoteli hiyo.

na Munir Zakaria, Zanzibar

 

 

 

VITENDO vya kishirikina vimeanza kuigubika sekta ya utalii visiwani humu kufuatia tukio la hivi karibuni, ambapo mwekezaji mmoja anayemiliki hoteli ya kitalii iliyopo katika eneo la Mji Mkongwe, kufanyiwa vitendo vya kishirikina ndani ya sebule ya hoteli hiyo.

 

Katika hali isiyotarajiwa, waliofanya vitendo hivyo ni Wazungu wawili, akiwemo mwanamke mmoja raia wa Marekani na mkazi wa Mbweni (jina tunalihifadhi), aliyefuatana na mwenzake wa kiume raia wa Afrika Kusini, anayeishi Mafia (jina tunalo).

 

Walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa watu hao walifika katika Hoteli ya Emerson Spice inayomilikiwa na Emerson Skeens, na kulazimisha kuingia ndani na kuwapuuza walinzi waliowauliza sababu ya wao kuingia katika hoteli hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea.

 

Wanaowafahamu watu hao, walilithibitishia gazeti hili kuwa nao wanamiliki hoteli ya kitalii katika eneo la Mji Mkongwe na kuna uwezekano mkubwa vitendo vyao hivyo vinalenga kumtisha mwekezaji huyo mpya atakayekuwa mshindani wao.

 

Baadhi ya mashuhuda waliieleza Tanzania Daima kuwa waliwaona Wazungu hao wakimwaga aina fulani ya unga, pamoja na maji katika sebule na pembe zote zinazozunguka hoteli hiyo inayojengwa.

 

Walisema kitendo hicho kiliwashangaza watu wengi kwa kuwa kilifanyika mchana saa nane, bila ya kuwa na woga wowote.

 

Mashuhuda walieleza kuwa baada ya kufika hapo, mwanamume ndiye aliyeingia ndani kwa hatua mbili na baadaye kutoka kizingitini kwa nje na kuinama na kugonga chini upande wa kulia na baadaye juu huku akisema maneno yasiyoeleweka.

 

Chanzo hicho cha habari kinadai kuwa kufuatia kitendo hicho, mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo pamoja na walinzi waliingilia kati na kuanza kumhoji wakitaka awaeleze kinagaubaga alikuwa akifanya nini.

 

Katika kujitetea, Mzungu huyo alikanusha kufanya vitendo vya kishirikina na badala yake alidai alikuwa akiizingua hoteli hiyo ili kuilinda na mazingira ya kichawi yanayoizunguka.

 

Baada ya mabishano makali, Mzungu huyo alilazimika kukimbia katika eneo hilo kwa lengo la kukwepa matatizo ambayo yangeweza kumkuta baada ya kuona kuwa waliomzunguka walianza kumtilia mashaka.

 

Skeens, ambaye ni raia wa Marekani, alithibitisha hoteli yake kufanyiwa vitendo hivyo, na kwamba tayari ameripoti kadhia hiyo katika Kituo cha Polisi Malindi kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.

 

“Mimi siamini uchawi wala ushirikina… namuamini Mungu tu, lakini matatizo haya yanatokana na kutokuwepo kwa Mahakama ya Biashara Zanzibar, ambayo ingesaidia kusikiliza kesi zinazotuhusu wawekezaji na hata wafanyabiashara,” alisema.

 

Alisema aliamua kufungua kesi polisi, ili ichukue hatua kwa wahusika ambao walikuwa na lengo la kumharibia biashara yake kwa kutumia nguvu za giza.

 

“Jambo la kushangaza sana, hawa waliofanya vitendo hivi ni watu waliosoma… mmoja daktari na mwenzake ni muuguzi, si jambo la kufurahisha kuona watu wenye elimu zao wanaendekeza vitendo vya kishirikina,” aliongeza kwa masikitiko.

 

Inadaiwa kuwa Mzungu aliyetenda vitendo hivyo alikimbia usiku wa tukio, ambapo siku ya pili mwenzake alipofuatwa nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alikiri kuwa rafiki yake aliondoka Zanzibar usiku uliopita, ambapo inadaiwa kuwa alikimbilia Mafia.

 

Ilielezwa kuwa mmiliki wa hoteli hiyo iliyofanyiwa vitendo vya ushirikina, alikuwa akimiliki hoteli nyingine ya kitalii iitwayo Emersdin & Green pamoja na Wazungu hao wawili, kabla hajajiondoa baada ya kutokea kutoelewana baina yao.

 

Baada ya kufarakana, alifungua kesi mahakamani kwa ajili ya kudai haki yake ya kuwa na hisa katika hoteli hiyo, ambayo alikuwa ni miongoni mwa wakurugenzi.

 

Hii ni mara ya kwanza kutokea vitendo vya kishirikina baina ya wawekezaji wenyewe tangu utalii ulipoanza kushika kasi na kuwa tegemeo la uchumi wa Zanzibar kutokana na kuchangia asilimia kubwa ya pato la taifa.

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents