BurudaniHabari

Wema Sepetu hoi Poland

WemaNdoto ya Watanzania kuendelea kutamba katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Dunia, ‘Miss World 2006’ juzi usiku ilipotea baada ya Wema Sepetu kuangukia pua katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika Warsal, Poland.

Wema Sepetu2006-10-02 08:46:38
By Majuto Omary na Mashirika

Ndoto ya Watanzania kuendelea kutamba katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Dunia, ‘Miss World 2006’ juzi usiku ilipotea baada ya Wema Sepetu kuangukia pua katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika Warsal, Poland.

Wema ameshindwa kutamba katika mashindano hayo na kuliachia taji la Miss World Africa kwenda kwa mrembo wa Angola, Stiviandra Oliveira.

Katika mashindano hayo, mrembo wa Ghana Inna Mariam Patty alitwaa taji la urembo wenye madhumuni maalum ”Beauty With A Purpose Award.”

Mwaka jana, Nancy Sumari aliitoa kimasomaso Tanzania kwa kutwaa taji hilo na kuwapa matumaini Watanzania kuwa ‘wataendelea’ kuling’ang’ania taji hilo mwaka huu.

Hata hivyo, mambo yamekuwa kinyume kabisa na Wema kujikuta miongoni mwa warembo 11 wa Tanzania walioshindwa kutamba katika mashindano hayo.

Warembo ambao wamefanya vibaya katika mashindano hayo ni; Aina Maeda Tanzania mwaka 1994, Emily Adolph (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998) na Hoyce Temu (1999).

Wengine walioambulia patupu kwenye mashindano ya Dunia ni Jacqueline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003) na Faraja Kotta (2004).

Watanzania walionyesha ‘wasi wasi’ kwa Wema mara baada ya taarifa kuwa mrembo huyo hakushinda hata taji moja la awali.

Baadhi ya wadau wa urembo walisema kuwa hilo ni pigo kubwa kwa mrembo huyo na kutilia wasiwasi kama kweli atatetea taji la Nancy au kufanya vyema zaidi ya Nancy.

Katika kinyang’anyiro hicho, Tatana Kucharova (18) wa Jamhuri ya Czech ambaye ni mwanafuzi alitwaa taji la dunia na kuwashinda warembo wengine 103 walioshiriki mashindano hayo.

Kucharova alipigiwa kura nyingi na majaji na watazamaji wa televisheni.

Mshindi wa pili wa mashindano hayo ya 56 ni Joana Valentina Boitor, kimwana mwenye umri wa miaka 17 kutoka Romania na mlimbwende wa Australia, Sabrina Houssami (20) ameshika nafasi ya tatu.

Tatana Kucharova hakuweza kujizuia kulia baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa mashindano hayo mara baada ya kuvishwa taji la almasi kutoka kwa Miss World wa mwaka jana, Unnur Birna Vilhjalmsdottir wa Iceland.

Kucharova alitoa ishara ya busu kwa watanzamaji 2,500 wa mashindano hayo huku akiwakumbatia washiriki wengine.

Kucharova ni mrembo wa tatu kutoka Ulaya Mashariki kushinda taji hilo. Mrembo wa kwanza alikuwa Aneta Beata Kreglicka wa Poland.
Source: Nipashe

{mos_sb_discuss:14}

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents