Habari

Wezi wa mafuta ya transfoma ni TANESCO wenyewe – Mbunge

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya, amesema wezi wa mafuta ya transfoma za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ni wafanyakazi wenyewe wa shirika hilo.

na Christopher Nyenyembe, Mbeya

 

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya, amesema wezi wa mafuta ya transfoma za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ni wafanyakazi wenyewe wa shirika hilo.

 

Mbunge huyo ameamua kutoboa siri hiyo kutokana na giza nene linaloendelea kuwakumba baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na ongezeko la wizi wa mafuta ya transfoma, huku akiwa mmoja wa waathirika na hali hiyo.

 
Mpesya anayeishi eneo la Iganzo, amekuwa miongoni mwa wakazi wa jiji wanaolala gizani kutokana na hujuma inayofanywa na wananchi wanaoliibia shirika hilo mafuta hayo na kuziacha transfoma zikilipuka.

 
Kutokana na wizi huo, Mpesya ameamua kuweka hadharani ukweli wa hujuma hizo kwa kudai kuwa, wanaohusika na njama hizo dhidi ya shirika hilo ni wafanyakazi wenyewe wa TANESCO na si vinginevyo.

 
Katika mahojiano yake na Tanzania Daima juzi, mbunge huyo ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge iliyokuwa mkoani hapa kukagua shughuli mbalimbali za kiusalama, alisema hakuna mwananchi wa kawaida anayefaya wizi huo isipokuwa ni wafanyakazi wenyewe wa TANESCO.

 
“Nimepewa taarifa na baadhi ya wananchi kuwa, wanaohusika na wizi huo ni wafanyakazi wa TANESCO na ndio wenye vifaa vya kupanda kwenye nguzo wakiwa na gloves, ngazi za TANESCO na vifaa maalumu vya kufungulia transfoma, hakuna watu wengine,” alisema Mpesya.

 
Aliyataja maeneo mengine yaliyokumbwa na wizi huo kuwa ni Isanga, Iganzo Tankini na Iganzo kwa Mbunge ambako transfoma tatu zimeibwa mafuta na hivyo kuwafanya wananchi wa maeneo hayo waishi gizani.

 
Alisema hali ya usalama katika Jiji la Mbeya hivi sasa inatia shaka na kuashiria kuongezeka kwa matukio ya uhalifu, hasa kutokana na giza lililotanda kwenye mitaa kadhaa jijini hapa kutokana na wizi wa mafuta ya transfoma kuzidi kuongezeka.

 
Mpesya alisema umefika wakati ambao wananchi katika mitaa yao wanapaswa kupewa jukumu la kuzitunza na kuzilinda transfoma hizo na hatakiwi mtu yeyote anayejifanya mfanyakazi wa shirika hilo kupanda kwenye nguzo bila kukutana na uongozi wa mtaa ili wafahamu kitu kinachotakiwa kufanywa.

 
Pia aliushauri uongozi wa shirika hilo kufanya utafiti wa kina unaohusu matumizi ya mafuta hayo licha ya kuwepo kwa watu wengi wanaodai kuwa yanatumiwa kukaangia chipsi, lakini alielezea wasiwasi wake akidai kuwa inaonekana yana kazi nyingine zaidi na ndiyo maana wizi huo haukomi.

 
Hivi karibuni, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mbeya, Deogratias Ndamugoba alisema katika kipindi kifupi, zaidi ya transfoma sita ambazo gharama yake halisi bado haijafahamika, zimeungua kutokana na wizi wa mafuta.

 
Meneja huyo alisema kutokana na hujuma hiyo, maeneo kadhaa yatakosa umeme kwa muda usiojulikana kutokana na kukosekana kwa transfoma za akiba na kukosa mafuta hayo.

 
“Hata makao makuu Dar es Salaam tumewasiliana nao hawana transfoma za akiba. Tanzania hatuna mafuta maalumu kwa transfoma, kwa hiyo maeneo mengi yataathirika, wateja waliokuwa wakizitegemea transfoma hizo watakosa huduma ya umeme kwa muda mrefu,” alisema meneja huyo.

 
Ndamugoba aliwaomba wananchi watoe ushirikiano katika kuwadhibiti wahalifu hao na kwamba mtu yeyote atakayeonekana akijishughulisha kwenye transfoma bila gari la TANESCO, akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents