Habari

Wivu waleta msiba mzito

Wivu wa kimapenzi baina ya wawili wapendanao umeleta msiba mzito Jijini ambapo mtu mmoja ameuawa kinyama kwa kucharangwa mapanga huku mwingine akiwa taaban katika wodi mojawapo ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI.

Na Moshi Lusonzo

 
Wivu wa kimapenzi baina ya wawili wapendanao umeleta msiba mzito Jijini ambapo mtu mmoja ameuawa kinyama kwa kucharangwa mapanga huku mwingine akiwa taaban katika wodi mojawapo ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI.

 

Aliyeuawa kwa kucharangwa mapanga na kupigwa mawe na wananchi wenye hasira, ni mmoja kati ya wapambe wa mume huku mpambe mwingine akilazwa kutokana na majeraha mazito aliyoyapata mwili mzima.

 

Wakizungumzia tukio hilo lililojiri hivi karibuni katika maeneo ya Tabata Kimanga na kisha polisi kulitolea taarifa, mmoja wa mashuhuda amesema vipigo vilivyotolewa na wananchi wenye hasira vilikuwa vya kutisha kwelikweli.

 

Akisimulia zaidi, mmoja kati ya mashuhuda hao amesema aliyefariki amefahamika kwa jina moja la Amiru huku mwingine aliyejeruhiwa na kulazwa Muhimbili akitambulika kwa jina la Kankuru Severine, 25.

 

Wanasema mashuhuda kuwa tukio hilo, limewakumba wahusika wakati walipokwenda na rafiki yao aitwaye Makongoro, kufanya fumanizi lililomhusisha mke wa rafiki yao huyo (Makongoro) waliyemtuhumu kuwa anachukuliwa kimapenzi na mwanaume mwingine Julius Jonas huko Tabata.

 

Wakasema, safari za marafiki hao wenye miili ya kibaunsa ilianzia eneo la Kariakoo.

 

Hata hivyo, imedaiwa kuwa mara walipofika katika nyumba waliyohisi kuwa mwanamke huyo amewekwa kimada, walishuka na kwenda kugonga mlango ili kuendesha zoezi hilo.

 

Inaelezwa kuwa wakati walipokuwa wakigonga, ghafla alitokea mwanaume anayedaiwa kupora mwanamke huyo na hapo ndipo yalipotokea mabishano makali kabla wapambe hao mabaunsa hawajaanza kutembeza kipigo.

 

“Kulikuwa na mabishano kati ya pande mbili, yule bwana alikataa kuwaingiza ndani huku watu hao walimlazimisha waingine ndani ili kumchomoa yule mwanamke,“ akasema mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka kutaja jina lake.

 

Baada ya kuona hali imekuwa ngumu mwanaume huyo anadaiwa kuwaitilia wezi jamaa na ndipo wananchi kibao walipojitokeza huku wakiwa na mapanga, mawe na silaha nyingine kadhaa.

 

Inaelezwa kuwa baada ya hapo, wananchi hawakutaka kuuliza na kwa hasira wakaanza kuwachangamkia wapambe hao kwa kipigo kabla ya kumuua mmoja na kumjeruhi vibaya mwingine aitwaye Severine.

 

“Kama isingelikuwa polisi kuwahi kwenye eneo hilo, nadhani hivi sasa tungeongea mengine kwa huyu Severin, kama ilivyokuwa kwa mwenzie,“ akasema shuhuda huyo.

 

Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa amesema Severine alifikishwa hapo akiwa hoi, huku sehemu kubwa ya maungo yake yakiwa yameathirika kwa kupigwa mapanga na silaha nyinginezo.

 

“Hivi sasa ana nafuu kulinganisha na hali aliyokuwa nayo wakati akifikishwa… madaktari wanaendelea kumpa huduma,“akasema Bw. Jumaa.

 

Aidha, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Faustine Shilogile, amelielezea tukio hilo kuwa limetokana na fumanizi.

 

Amesema watu hao wanaodaiwa kuwa ni mabaunsa, walimvamia mtu huyo kwa madai kuwa alikuwa akiishi na mke wa mmoja wa rafiki yao.

 

Amesema tukio hilo limetokea siku ya Jumatatu mishale ya saa 4:00 asubuhi.

 

Hatahivyo, hakukuwa na taarifa rasmi juu ya mahala alipo mume wa huyo mwanamke anayetajwa kwa jina la Makongoro wala mke mwenyewe.

 

 

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents