Fahamu

Yafahamu mataifa yanayotajwa ni hatari zaidi kusafiri kwa ndege duniani, Afrika latajwa taifa hili

Yafahamu mataifa yanayotajwa ni hatari zaidi kusafiri kwa ndege duniani, Afrika latajwa taifa hili

Usafiri wa ndege ni moja ya njia salama zaidi za kusafiri duniani, lakini katika baadhi ya mataifa yenye mifumo dhaifu ya usimamizi wa safari za ndege pamoja na ukosefu wa miundo mbinu bora, unaweza kuwa hatari.

Ajali mbili za ndege zilizotokea majuzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeibua maswali kuhusu usalama katika uchukuzi wa angani katika taifa hilo la Afrika ya kati.

Ajali ya majuzi zaidi ilitokea wikendi iliyopita ambapo ndege ilianguka katika eneo la makazi katika jiji la Goma, mashariki mwa nchi hiyo, na kuua watu 27.

Lakini je, usafiri wa ndege DR Congo ni hatari kiasi gani, na taifa hilo likoje ukilinganisha na mataifa mengine duniani?

Usalama wa uchukuzi wa ndege DR Congo

Takwimu kutoka kwa Aviation Safety Network, shirika linalofuatilia na kukusanya taarifa na maelezo kuhusu usalama wa safari za ndege, zinaonyesha kwamba DR Congo imeshuhudia ajali nyingi zaidi za ndege za kubeba abiria barani Afrika tangu 1945.

Rescue workWaokoaji wakijaribu kufikia walioathirika na mkasa wa ndege Goma hivi majuzi

Dkt Daniel Kwasi Adjekum kutoka Chuo Kikuu cha Dakota Kaskazini nchini Marekani anasema kuwepo kwa ajali nyingi za ndege DR Congo kunachangiwa na sababu kadha ikiwemo ukubwa wa taifa hilo, mandhari ya nchi na mifumo dhaifu ya usimamizi wa safari za ndege.

Uchukuzi wa angani ni muhimu sana katika taifa hilo ikizingatiwa kwamba ndiyo njia pekee ya kutegemea kufika baadhi ya maene.

Kati ya miji mikuu ya mikoa 25 nchini humo, ni miji minne pekee ambayo unaweza kusafiri kwa uhakika kwa kutumia barabara kutoka mji mkuu Kinshasa.

Lakini DR Congo ina miundo mbinu iliyochakaa katika viwanja vya ndege na mitambo ya kufuatilia na kuongoza safari za ndege. Sheria na mifumo ya kiufundi ya kusimamia uchukuzi wa angani pia ni dhaifu.

Taifa hilo linakabiliwa na changamoto pia kutokana na matumizi ya teknolojia zilizopitwa na wakati na pia matumizi ya ndege zilizoundwa miaka mingi iliyopita ambazo si imara tena na mifumo yake si ya kisasa.

Mataifa yaliyoshuhudia ajali nyingi zaidi za ndege

Tangu 2010 hadi sasa.

Chanzo: The Aviation Safety Network

Kuna tatizo pia kutokana na wahudumu wa ndege na pia wafanyakazi wa kukagua na kukarabati ndege ambayo hukosa watu wa kufuatilia utendaji kazi wao na pia hakuna viwango na kanuni kali za kufuatwa.

Baadhi ya ajali hata hivyo husababishwa na sababu zisizoepukika kama vile mazingira.

Mfano ni hali ya hewa ambapo mvua kubwa na ukungu wakati mwingine huathiri safari za ndege. DR Congo huwa katika ukanda wa tropiki ambapo mvua kubwa hunyesha mara kwa mara katika maeneo mengi.

Duniani taifa gani linaongoza kwa ajali?

Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuwa na ajali nyingi zaidi za ndege tangu mwaka 2010, ikifuatwa na Urusi, Canada, mexico na Indonesia.

Lakini Marekani pia inaongoza kwa kuwa na ndege nyingi zaidi ambazo hupaa katika anga yake kwa hivyo kimsingi unaweza kutarajia ajali ziwe nyingi huko.

Kwa idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali za ndege, watu 532 wamefariki nchini Urusi tangu 2010 ambayo ndiyo idadi ya juu zaidi duniani.

Taifa la Indonesia linafuata kwa vifo vya watu 520 katika kipindi hicho.

Waliofariki kutokana na ajali za ndege

Tangu 2010 hadi sasa

Chanzo: Aviation Safety Network

Mataifa hayo mawili kwa sasa yana idadi kubwa ya ndege zinazopaa na idadi hiyo imeendelea kuongezeka sana katika mwongo mmoja uliopita.

Nchini Urusi, idadi ya watu wanaosafiri kwa kutumia ndege imeongezeka mara tatu tangu mwaka 2009 na nchini Indonesia idadi hiyo imeongezeka mara nne.

Idadi ya watu waliofariki nchini DR Congo kutokana na ajali za ndege ni karibu sawa na taifa kama Nepal katika bara Asia taifa ambalo pia lina mandhari magumu yenye milima mirefu.

Nepal pia ina changamoto kubwa katika kudhibiti safari za ndege, kuhakikisha usalama wa uchukuzi wa angani na pia idadi ya watu wanaotumia ndege kusafiri imekuwa ikiongezeka.

Kupigwa marufuku

Rekodi mbaya ya usalama wa usafiri wa ndege nchini DR Congo imelifanya taifa hilo kuwa miongoni mwa nchi ambazo mashirika yake yote ya ndege hayaruhusiwi kuingiza ndege katika anga ya Umoja wa Ulaya, au mashirika hayo yamewekewa vikwazo.

Lakini taifa hilo silo pekee kutoka Afrika katika orodha hiyo.

A plane in DR Congo which overshot the runway

Orodha hiyo ina mataifa mengine 13 ya Afrika, pamoja na baadhi ya mataifa ya Asia na Amerika Kusini.

Nchini DR Congo, mwaka mbaya zaidi kwa ajali za ndege ulikuwa mwaka 2007 ambapo kulitokea ajali nane za ndege katika kipindi cha mwaka mmoja.

Lakini ajali mbaya zaidi ya ndege nchini DR Congo ilitokea mwaka 1996 pale ndege ya kusafirisha mizigo ilipopoteza njia ikijaribu kupaa na kuingia kwenye soko lililojaa watu na kuua watu 237.

Chanzo BBC.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents