Yanga yawaliza Wacanada

Yanga yawaliza Wacanada
Wawakilishi wa Tanzania Bara katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika Yanga, jana walionyesha makali yao baada ya kuifunga Vancouver Whitecaps kwa bao 3-0, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga inayojiandaa kucheza na Al Ahly ya Misri katika ligi ya Mabingwa wa Afrika, iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 37 lililowekwa kimiani na Jerry Tegete baada ya kupokea pasi ya Shamte Ally, na kumpiga chenga kipa Nally Jay kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Dakika tatu baadae, Yanga iliongeza bao la pili mfungaji akiwa ni Tegete tena baada ya kuunganisha krosi ya Shadrack Nsajigwa.

Mkenya Ben Mwalala alihitimisha ushindi wa Yanga kwa kufunga bao la tatu katika dakika ya 51 baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Vancouver.

Hatahivyo, timu hiyo ya Canada muda mwingi wa mchezo huo ilicheza pungufu baada ya mchezaji wake mmoja, Burges Tyrell kutolewa nje baada ya kumchezea vibaya Amir Maftah.

Kocha wa Yanga Mserbia Kondic alisema kuwa timu yake ilicheza vizuri na aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo, lakini alionya kuwa usichukuliwe kama ni kipimo kizuri kwa ajili ya wapinzani wao wa Misri Al Ahly itakayocheza nayo hivi karibuni katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Yanga Obreni Curkovic/Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Nadir Haroub `Canavaro`, George Owino, Wisdom Ndlovu, Shamte Ally/Mike Barasa, Abdi Kassim/Ben Mwalala, Nurdin Bakar, Jerry Tegete na Athumani Idd.

 

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW