Habari

Zaidi ya Wayemeni milioni 20 wakabiliwa na balaa la njaa, Umoja wa mataifa waingilia

Umoja wa Mataifa umesema watu milioni 20 nchini Yemen wanakabiliwa na baa la njaa, hiyo ikiwa asilimia 70 ya idadi ya raia wa taifa hilo linalokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mkuu wa shirika la kutoa misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 15 ya idadi ya Wayemeni waliokuwa wakikumbwa na njaa mwaka jana na kuonya kuwa hali ya kibinadamu nchini humo inazorota kwa kasi kubwa na inatia wasiwasi mkubwa.

Lowcock amesema kwa mara ya kwanza raia 250,000 wa Yemen wanakabiliwa na kile alichokitaja janga linalowaweka katika hatari ya kufa njaa.

Mamilioni wako hatarini kufa njaa

Kwa mujibu wa DW Swahili, Umoja wa Mataifa unasema kiwango hicho cha njaa kiko katika kiwango cha tano ambacho ni cha juu zaidi cha watu wanaorodheshwa kuwa na uhaba mkubwa mno wa chakula na kukumbwa na utapia mlo wa kiwango cha juu sana. Nchi nyingine duniani ambayo imewekwa katika kiwango cha tano cha njaa ni Sudan Kusini ambayo watu 25,000 wako katika hatari ya kufa njaa. Majimbo yaliyoathirika zaidi Yemen ni Taiz, Saada, Hajja na Hodeida ambayo yanashuhudia mapigano makali. Mzozo wa Yemen ulianza mwaka 2014 wakati wa waasi wa Houthi walipoudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa na kuipindua serikali ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati kijeshi mzozo huo ili kuisadia serikali ya Hadi kwa kupambana na Wahouthi mwaka 2015.

Wanaoathirika zaidi ni raia ambapo zaidi ya 10,000 wameuawa tangu wakati huo na mamilioni wakikumbwa na mzozo wa kibinadamu unaotajwa kuwa mbaya zaidi duniani.

UN yahitaji dola bilioni 4

Umoja wa Mataifa umesema unahitaji dola bilioni 4 kutoa misaada ya kibinadamu kwa Wayemeni hao milioni 20 wanaokumbwa na baa la njaa mwaka ujao. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataongoza mkutano wa wafadhili kwa ushirikiano na Sweden na Uswisi mjini Geneva mnamo tarehe 26 mwezi Februari. Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimeahidi kutoa dola milioni 500. Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya kiutu Mark Lowcock amesiistiza kuna mambo matano yanayohitajika ili kurejesha uthabiti Yemen, nayo ni kusitishwa kwa mapigano katika mji wa bandari muhimu wa Hodeida ambako asilimia 70 ya chakula na mahitaji mengine huingizwa kupitia bandarai hiyo.

Kupunguza vikwazo dhidi ya mashirika ya kutoa misaada na kuingizwa kwa mafuta, mambo ambayo yanahitajika sana, kuufanya uchumi wa Yemen ulioporomoka kutokana na vita kuwa thabiti.

Hivi sasa serrikali inakusanya asilimia 15 tu ya mapato, kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kuchangisha dola bilioni 4 ili kuwasaidia Wayemen na hatua madhubuti kuendelea kuchukuliwa kati ya serikali na waasi wa Houthi katika meza ya mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents