Zanzibar gizani siku ya 19 sasa

Imebainika kuwa Chanzo cha kuungua na kuharibika waya wa umeme wa chini ya bahari unaopeleka umeme Zanzibar kuwa ni ukosefu wa betri za kuendeshea jenereta za kupoza waya huo ambao unalazimika kupozwa….

zanzibar_1.jpg

 

Imebainika kuwa Chanzo cha kuungua na kuharibika waya wa umeme wa chini ya bahari unaopeleka umeme Zanzibar kuwa ni ukosefu wa betri za kuendeshea jenereta za kupoza waya huo ambao unalazimika kupozwa muda wote bila kujali unazalisha umeme ama umezimwa.

Habari kutoka ZECO zilieleza kuwa ni uzembe na urasimu mkubwa sababu umeme wa gridi ya taifa unaopokelewa katika mitambo ya Ras-Fumba, kulipuka kutokana na mashine maalum ya kupozea waya wa baharini unaotoka Bara kuja Zanzibar kushindwa kufanyakazi baada ya umeme kukatika Mei 21 mwaka huu.

Imeelezwa kuwa kituo hicho kina mashine maalum za kupozea waya huo unaopokea umeme wa gridi ya taifa kutoka Kidatu mkoani Morogoro ambazo siku zote hupoza waya huo hata kama umeme umekatika au unawake.

Mara nyingi ikiwa umeme umekatika mashine hizo hufanyakazi ya kuupoza waya huo kwa kutumia jenereta lakini kama kuna umeme mashine za kuupoza nazo hutumia umeme.

Taarifa hizo kutoka ZECO zilieleza kwamba miezi mwili kabla ya Zanzibar kukosa umeme uongozi wa kituo cha Ras-Fumba uliandika barua kuomba Sh.150,000 kwa ajili ya kununulia betrii mpya za jenereta zinazowashwa kupoza waya huo endapo umeme utakatika ili nazo zifanye kazi hata kama waya haupokei umeme kwani hilo ni moja la sharti la waya huo.

Lakini habari zaidi zilisema kuwa fedha hazikutolewea hadi mlipuko ulipotokea Mei 21 na habari ziliongeza kuwa siku ya pili -Mei 22 uongozi wa ZECO ulinunua betrii hizo na kuzipeleka katika kituo hicho. Hata hivyo hazikusaidia kitu na hadi leo umeme haujapatikana huku uchumi wa nchi na huduma za jamii vikiwa kwenye hati hati.

Chanzo hicho cha habari kilisema umeme unapokuwepo mashine hizo huendeshwa na umeme lakini unapokatika jenereta hutumika kupoza waya huo wenye nguvu ya kilovolti 132.

Taarifa zaidi zilisema kukosekana betrii hizo ili kuwasha jenereta ya kupoza waya kulisababisha kazi ya kupoza waya huo isifanyike na waya huo kuungua na kuiacha Zanzibar gizani. Hivi karibuni mtaalamu wa umeme kutoka Norwey akifafanua suala hilo kwa Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Bw.

Ali Juma Shamuhuna, alisema chanzo cha kukatika umeme huo ni baada ya umeme kurejea ukiwa na nguvu kubwa na kusababisha waya huo kulipuka.

Mtaalamu Nexans ya Norway, Bw. Haakon Hamre, Hata hivyo alisema matumaini ya kutengenezwa eneo hilo na umeme kurejea upo lakini akaonya kuwa kunahitajika umakini mkubwa katika kazi hiyo na katika kutunza vifaa hivyo.

Kauli ya mtaalamu huyo inatofautiana na ya Meneja Mkuu wa ZECO Bw. Juma Isihaka. ambaye awali alisema umeme baada ya kurejea ulikuwa na nguvu ya kiwango cha chini cha kilovolti 15.

Ofisa Uhusiano wa ZECO Bw. Salum Abdallah, alipinga uwepo urasimu na uzembe katika tukio hilo na kusababisha kucheleweshwa kununuliwa betrii hadi mitambo ikalipuka .

Aliongeza kuwa ZECO inashughulikia tatizo la Ras-Fumba kwa kufanya matengezo ya mara kwa mara na kamwe hakuna uzembe uliojitokeza na kusababisha Zanzibar kuwa gizani.

Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi Bw. Mansour Yussuf Himid, alisema serikali inaamini sababu ya kulipuka kwa waya huo ni zile zilizotolewa na mtaalamu wa Norway.

Zanzibar iko gizani kwa siku 19 leo hali iliyosababisha uhaba mkubwa wa maji, kuathiri uzalishaji viwandani na katika huduma hasa sekta ya utalii na hospitali. ZECO hadi sasa imeshapoteza zaidi ya Sh milioni 500 kutokana na kukosa mapato ya milioni 30 kila siku.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents