Habari

Zanzibar waikataa sheria ya rushwa

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema sheria mpya ya kupambana na rushwa, iliyopitishwa na Bunge juzi jioni, haitafanya kazi Zanzibar kwa vile hilo si suala la Muungano.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima, Zanzibar


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema sheria mpya ya kupambana na rushwa, iliyopitishwa na Bunge juzi jioni, haitafanya kazi Zanzibar kwa vile hilo si suala la Muungano.



Hayo yalisemwa jana na Mwasheria Mkuu wa SMZ, Idd Pandu Hassan, alipokuwa akizungumza na Tanzania Daima, katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi mjini Unguja.



Alisema kwamba, ili sheria hiyo iweze kufanya kazi visiwani humu, ni lazima ipate baraka za SMZ na baadaye kuridhiwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.



Kauli hiyo ya Pandu, kwa maana nyingine, inaongeza utata katika masuala yanayohusu Muungano, hasa ikizingatiwa kuwa, Bunge la Jamhuri ya Muungano lililopitisha sheria hiyo juzi, lina wawakilishi kutoka majimbo yote ya Unguja na Pemba.


Kwa upande wake, Pandu alisema masuala ya rushwa si ya Muungano, hivyo serikali mbili lazima zishauriane juu ya sheria hiyo, kabla ya kufanya kazi Zanzibar.



Alisema hayo baada ya baadhi ya wabunge, wakiwamo wale wa kutoka Zanzibar, kushauri sheria hiyo ihusishe na Zanzibar, kwa vile pia kuna tatizo kubwa la rushwa.


Wabunge hao walisema kwamba, kwa kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, si vizuri sheria hiyo kuitenga Zanzibar, kama serikali kweli imeamua kupambana na rushwa.



Hata hivyo, wakati Zanzibar ikihoji kuhusu hilo, hivi karibuni SMZ ilieleza kuridhia kupokea mamilioni ya fedha za mikopo kwa wajasiriamali, zilizotolewa na serikali na kupitishwa na Bunge pasipo kuhoji iwapo uamuzi huo ulikuwa wa upande mmoja.



Tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, wamekuwa wakikutana kuzungumzia kile kinachojulikana kuwa matatizo ya Muungano.



Hivi karibuni, rasimu ya sheria ya mamlaka ya kupambana na rushwa na kuweka maadili ya viongozi, ilikwama kupitishwa na Baraza la Mawaziri kwa madai kuwa, ilikuwa bado haijaiva na nchi ilipaswa kuchukua uzoefu katika nchi za Jumuiya ya Madola.



Hadi sasa, rasimu hiyo imewasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri zaidi ya mara tatu, lakini wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, wameambiwa bado haijaiva tayari.



Aidha, baraza hilo la mawaziri, liliwataka maofisa hao kuchukua uzoefu huo katika nchi za Jumuiya ya Madola, badala ya kuchukua katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania Bara pekee.



Rasimu hiyo imependekeza adhabu nzito kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Aidha, inawalazimisha wanasiasa na viongozi watakaoteuliwa na rais, kutangaza mali zao mara wanapoingia madarakani na wakati wakimaliza muda wao.



Mbali na viongozi hao, watoto wao pia wanapaswa kutangaza mali walizonazo ili kupata kumbukumbu nzuri za mali wanazomiliki pale wazazi wao, wanapomaliza muda wao.



Aidha, sheria hiyo inawabana viongozi wa kisiasa kujiepusha na kutoa takrima, ikiwemo huduma ya malazi na viburudisho wakati wa uchaguzi.



Katika muswada huo, imependekezwa adhabu ya faini ya sh milioni 10 au kifungo cha miaka 10 kwa mtu yeyote atakayepatikana na makosa ya kupokea au kutoa rushwa.



SMZ haijasema ni lini wataalamu wa Zanzibar watatumwa katika nchi hizo za Jumuiya ya Madola ili wakachukue uzoefu wa sheria kama hiyo, lakini wataalamu kutoka katika Ofisi ya Katiba na Utawala Bora, wamekuwa wakizunguka na rasimu hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents