Zanzibar wapinga viwango vipya vya umeme

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepinga kutumika kwa viwango vipya vya umeme kama vilivyopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa bei za Maji na Nishati (EWURA)

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepinga kutumika kwa viwango vipya vya umeme kama vilivyopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa bei za Maji na Nishati (EWURA).

Wajumbe hao wamesema endapo viwango hivyo vipya vitaanza kutumika, Zanzibar itaathirika kiuchumi na wananchi wengi watalazimika kurejea katika matumizi ya kuni na vibatari.

Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi, Wajumbe hao walisema umefika wakati kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano na SMZ, kukutana na kujadili suala hilo baada ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kutishia kukata huduma hiyo endapo Zanzibar itashindwa kuheshimu viwango vipya vya bei.

Mwakilishi wa Jimbo la Koani (CCM), Bw. Haji Mkema alisema Zanzibar itaathirika kiuchumi iwapo itavikubali viwango vipya na kuongeza kuwa uchumi wa Zanzibar na Bara unatofautiana na watakaoumia ni wananchi wa kawaida.

“Viwango hivi ni vikubwa sana kwa Zanzibar na watakaoumia ni wananchi wa kawaida kwa vile kipato cha wananchi baina ya Zanzibar na Bara vinatofautiana, ndio maana tunasema viongozi wakuu wakutane kujadili suala hili kabla halijafikia katika hatua mbaya,“ alisema Bw. Mkema.

Bw. Mkema alisema hivi sasa Zanzibar inaendelea na utekelezaji mradi wa umeme vijijini, na iwapo viwango hivyo vitapitishwa umeme huo utabakia kama mapambo kwa vile wananchi wengi hawatoweza kumudu gharama na badala yake kutumia nishati ya kuni na vibatari.

Naye Mwakilishi wa jimbo la Magomeni (CCM) Bw. Salmin Awadh alisema EWURA wamekiuka mkataba wa Tanesco na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa vile kabla ya kupandishwa kwa bei mashirika hayo yalipaswa kupewa nafasi ya kujadiliana kama utaratibu uliokuwa ukitumika katika miaka ya nyuma.

“Masuala haya yalihitaji mazungumzo baina ya pande mbili za Muungano kabla ya Zanzibar kupandishiwa bei ya umeme, kwa vile mashirika haya ni ya umma na Serikali zote mbili zina dhamana kubwa kutokana na umuhimu wake,“ alisema Bw. Salmin.

Alisema sera ya uhifadhi mazingira ya Zanzibar itaathirika kwa vile viwango vipya vilivyotangazwa vitasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na gharama za umeme kuelekea kupanda kwa zaidi ya mara tatu ya viwango vya sasa.

Mwakilishi huyo alisema Tanesco hawakutumia kitendo cha busara kwa kutishia kuikatia umeme Zanzibar kwa vile msimamo huo umekuja siku chache tangu Zanzibar ilipokuwa katika kipindi kigumu cha ukosefu wa umeme kilichodumu kwa siku 28.

“Tanesco hawakutumia lugha nzuri kutishia kuikatia umeme Zanzibar, sote tunaelewa kuwa Zanzibar ni sehemu ya Muungano na siasa za muungano lazima ziheshimike, kwa vile suala la umeme ni huduma inayohusu wananchi wa pande zote,“ alisema Mwakilishi huyo.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chake chake Pemba Bw. Ali Omar alisema kwamba kitendo cha Tanesco kutangaza kuikatia umeme Zanzibar ni cha kuidhalilisha Zanzibar na viongozi Tanesco wanapaswa kuwaomba radhi wananchi wa Zanzibar.

Alisema kimsingi Zanzibar ilipaswa kushirikishwa katika mchakato wa upangaji wa viwango vipya vya bei, kwa kuwa ingesaidia kufahamu vigezo vilivyotumika vya Zanzibar kupandishiwa bei kwa asilimia 168 na Tanzania Bara asilimi 21.7.

“Kinachotushangaza wenzetu wa Bara wana uchumi mkubwa tofauti na Zanzibar lakini wamepandishiwa umeme kwa asilimia 21.7, na bado wanatoa vitisho vya kukata umeme, na ndio maana tunauliza menejimenti ya Tanesco inawatakia kheri wananchi wa Zanzibar,“ alihoji Mwakilishi huyo.

Alisema wakati umefika kwa Waziri Mkuu Bw,Mizengo Pinda na Waziri Kiongozi, Bw. Shamsi Vuai nahodha kuchukua hatua ya kutafuta ufumbuzi wa tatzizo hilo kabla ya tishio la kukatwa na umeme halijaanza kutekelezwa na menejimenti ya Tanesco.

“Tatizo kubwa hawakuangalia Zanzibar kama ni mdau wa Muungano, isitoshe unaipandishia viwango vikubwa bila ya kufanya tathmini ya hali ya wananchi wake ambao wengi hawana ajira wala vyanzo vya uhakika vya kujipatia mapato,“ alisema Mwakilishi wa viti maalum wa CUF Bi. Zakia Omar.

Bi. Zakia alisema sehemu kubwa ya umeme Zanzibar inatumika kwa huduma ya majumbani na maofisini kutokana na ukosefu wa viwanda, hivyo walipaswa kuzingatia hali hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi Zanzibar, Bw.Tafana Kassim Mzee aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba endapo Zanzibar itafuata viwango hivyo vipya vya umeme italazimika kutumia bilioni 3.2 kwa mwezi kwa ajili ya kununua umeme kutoka Tanesco badala ya milioni 900 zinazotumika hivi sasa.

Alisema Zanzibar imelazika kugoma kutumia viwango vipya kwa vile viwango hivyo vipya vitavuruga sekta ya utalii ambayo kwa sasa inaonekana kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.

“Kama tutumia viwango hivi sekta ya utalii itaathirika vibaya, kutokana na huduma kulazimika kupanda zaidi ya mara tatu ya viwango vya sasa, na tutakuwa kama tunawafukuza watalii, ambao wanatuingizia mapato mengi,“ alisema Naibu Waziri huyo.

Alisema Zanzibar imeamua kutumia viwango vya bei vinavyotumika Tanzania Bara vya asilimia 21.7 kitendo ambacho kinapingwa na menejimenti ya Tanesco ambapo Juni 27, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji Dk. Idrisa Rashidi alitishia kuikatia umeme Zanzibar endapo itashindwa kuheshimu viwango vipya vya bei ya umeme.

Alisema tangu waanze kutumia viwango hivyo vinavyotumika Tanzania Bara gharama za ununuzi wa umeme zimepanda kutoka shilingi milioni 900 hadi Sh. bilioni 1.2 kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema Zanzibar hivi sasa inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwa na umeme wa akiba ambapo alisema ifikapo mwaka 2009 Zanzibar itakuwa na chanzo cha umeme kitakachozalisha megawati 25 kupitia majenereta.

Naibu Waziri huyo alisema EWURA haina mamlaka ya kupanga viwango vya bei kwa upande wa Zanzibar kwa vile taasisi hiyo siyo ya Muungano na ndio maana TANESCO imekuwa ikishauriana na ZECO kabla ya kupandisha kwa bei ya umeme tangu kufikiwa kwa mkataba wa huduma mwaka 1979.

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents