Z`bar gizani siku 21

Wataalamu wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), jana walikwama kutatua tatizo la ukosefu wa umeme visiwani hapa kutokana na kukosa vitendea kazi

Na Joseph Mwendapole

Wataalamu wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), jana walikwama kutatua tatizo la ukosefu wa umeme visiwani hapa kutokana na kukosa vitendea kazi.

Kutokana na hali hiyo, mashirika hayo yamewaagiza wataalamu wake kufuata vifaa jijini Arusha wakati wakisubiri wataalamu wengine kutoka nchini Norway.

Akizungumza Visiwani hapa jana, Mhandisi wa Matengenezo kutoka TANESCO, Bw. Josephat Gandie, alisema zoezi la matengenezo limesimama hadi vifaa vitakapowasili.

“Hata hivyo tunazingatia pia ushauri wa Rais Amani Abeid Karume, aliyetuambia tufanye matengenezo kwa ushirikiano wa ZECO, TANESCO na Wanorway,“ alisema.

Alisema wakati wakiwasubiri wataalamu kutoka Norway, vifaa vimewakwamisha kazi hiyo kutokana na kutopatikana Zanzibar na kwamba tayari TANESCO wakishirikiana na ZECO, wameviagiza Arusha. Bw. Gandie, alisema wataalam kutoka nchini Norway, wanatarajiwa kuwasili leo au kesho tayari kwa kuanza matengenezo.

Ofisa Uhusiano wa ZECO, Bw. Salum Abdallah alisema kuwa kifaa kilichoharibika kinaitwa Submarine Cable na kitatengenezwa kwa wiki tatu nchini Norway.

“Tulipeleka picha kwa kampuni ya Neksans Ltd ya nchini humo ambayo wamesema kuwa, kifaa hicho kitaweza kukamilika baada ya wiki tatu kwa kuwa ni oda maalum tumekubaliana nao lakini tunaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha umeme unarejea,“ alisema.

Hata hivyo, maji yamekuwa tatizo kubwa visiwani hapa jambo lililosababisha wanafunzi kufanya biashara ya maji badala ya kuingia darasani wakati daladala zimeacha kubeba abiria na kuingia katika biashara hiyo.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi waliozungumza na Nipashe, ndoo moja ya maji inauzwa kati ya Sh. 500 hadi 1,000.

Aidha, wakazi hao wameishauri mamlaka ya maji visiwani hapa kufunga jenereta katika mitambo yao ili kuwanusuru na magonjwa ya mlipuko yanayo sababishwa na maji yasiyo salama.

Wamiliki wa hoteli za kitalii walisema wameshindwa kutoa huduma ipasavyo kwa kuwa wanatumia majenereta ambayo wanalazimika kuyawasha usiku na kuzima mchana kutokana na sababu za kiufundi.

Kwa upande wa benki, huduma za ATM zimekosekana na kuwalazimu wananchi kwenda hadi makao makuu ya benki kufuata huduma hiyo.

Kadhalika, biashara ya samaki imezorota kutokana na wateja kuhofia kununua kitoweo hicho kwa wingi kwa kuhofia kuharibika.

Baadhi ya walimu na wanafunzi waliozungumza na Nipashe walisema kuwa masomo ya ziada yameathirika kwa kuwalazimu kusoma kwa muda mfupi.

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents