Siasa

Zitto atuma waraka kwa JK

Zitto KabweHUKUMU ya mahakama kuruhusu watu kugombea nafasi za uongozi kama wagombea binafsi, imemsukuma Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha Watanzania wanaifaidi haki hiyo ya kidemokrasia

na Kulwa Karedia

HUKUMU ya mahakama kuruhusu watu kugombea nafasi za uongozi kama wagombea binafsi, imemsukuma Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha Watanzania wanaifaidi haki hiyo ya kidemokrasia.

Ili kuhakikisha kuwa suala la mgombea binafsi linaingizwa katika mifumo halali wa uchaguzi na sheria za nchi, Zitto amemwandikia Rais Jakaya Kikwete pamoja na Bunge, akionyesha dhamira yake ya kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema kuwa suala la mgombea binafsi limecheleweshwa mno na anadhamiria kuhakikisha kuwa linapewa msukumo ili Watanzania wapate uhuru wa kuwania nafasi za uongozi.

Katika barua hiyo ya Mei 19 ambayo Tanzania Daima imepata nakala yake, Zitto alisema utekelezaji wa uamuzi huo utabadilisha mfumo wa uchaguzi nchini na ili utekelezeke, yanahitajika marekebisho ya Katiba ya nchi na sheria za uchaguzi.

“Kwa barua hii, natoa taarifa kuwa nina nia ya kuwasilisha bungeni muswada wa sheria za kurekebisha Katiba ya nchi na sheria za uchaguzi, hivyo naomba wataalamu wa ofisi yako waniandalie muswada huo,” anasema Zitto katika barua hiyo.

Katika barua hiyo, anamkumbusha Rais Kikwete kuwa kwa mara ya kwanza alimwandikia barua Mei 31 mwaka jana, akimjulisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu wagombea binafsi na umuhimu wa kubadili mfumo wa uchaguzi, lakini hakupata majibu ya msingi.

“Katika barua yangu hiyo nilishauri umuhimu wa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wetu wa uchaguzi, ili kuendana na si tu hukumu ile ya Mahakama Kuu kuruhusu wagombea binafsi, bali pia kuweka mazingira ya kisiasa ambayo yanatoa fursa kwa vyama kushindana kwa mujibu wa sera zao na hivyo kuimarisha asasi hizo muhimu za kidemokrasia,” alisema Zitto.

Alisema anarudia kuandika barua kwa mara ya pili baada ya serikali kushindwa rufaa iliyokata kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoka mapema mwaka 2006.

“Narudia ushauri wangu kwa serikali kukubali kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchaguzi, ili kukabiliana na changamoto za sasa na za baadaye za kisiasa nchini kwetu, lengo likiwa ni kuimarisha mfumo wa vyama vingi,” alisema.

Alisema kama wana siasa hawatakuwa makini, maamuzi ya mahakama yanaweza kuudhoofisha mfumo wa vyama vingi nchini na demokrasia kuparaganyika kabisa.

“Hatari ninayoiona ni kuwa kuruhusu wagombea binafsi bila kuwa na mfumo unaohakikisha uimara wa mfumo wa vyama vingi, kunaweza kupeleka nchi kuongozwa na kundi dogo lisilo na udhibiti,” alisema Zitto katika barua hiyo.

Alisema anaishauri serikali isipoteze muda kwa ajili ya kukata rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa ya serikali dhidi ya kuruhusu wagombea binafsi katika nyadhifa za kisiasa.

Katika barua hiyo, Zitto amependekeza mapendekezo matano, akitaka Bunge liwe na aina zifuatazo za wabunge.

Alisema aina ya kwanza ya wabunge ni wabunge waliochaguliwa kuwakilisha mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mamlaka hizo sasa zitatamkwa na Katiba, nazo ni halmashauri za wilaya, manispaa na miji.

“Hivi sasa nchini kuna mamlaka za serikali za mitaa zipatazo 124 kwa upande wa Tanzania Bara, hivyo hapa tunaweza kupata wabunge 124 wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, kundi hili ni dhahiri wagombea wataruhusiwa kikatiba na sheria ya uchaguzi itaweka masharti ya ushiriki wao,” alisema Zitto.

Alisema kwa upande wa Zanzibar wabunge wa kuchaguliwa watokane na wilaya za kiutawala za sasa, ambapo jumla ya wabunge 10 watapatikana.

Pendekezo la tatu, ametaka wabunge wa mikoa kwa Tanzania Bara watakuwa sawa na idadi ya wabunge wanaotokana na mamlaka za halmashauri za wilaya, ambao idadi yao itakuwa 124.

“Kwa upande wa Zanzibar ili kulinda matakwa ya Katiba, idadi ya wabunge wanapaswa kutopungua 50 kama ilivyo sasa, wabunge 40 watatokana na kundi hili la wabunge wa mikoa,” alisema.

Alisema mikoa itagawiwa wabunge kutokana na uwiano wa wananchi waliojindikisha kupiga kura katika mkoa husika na mgawo huo utakuwa ukirejewa kila baada ya miaka kumi.

Pendekezo la nne, Zitto alisema ni wabunge wanawake, ambao watakuwa asilimia 30 ya wabunge wanaotokana na makundi matatu ya juu kwa mujibu wa mfumo wa sasa.

Wakati pendekezo la tano, mbunge huyo kijana alisema ni wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Spika kama si mbunge.

“Ndugu Rais kwa mapendekezo haya tunaweza kutoa uhuru kwa raia wa Tanzania mwenye sifa na bila kujali kama ni mwanachama au si mwanachama wa chama cha siasa kugombea ubunge na hata udiwani,” alisema.

Alisema mapendekezo hayo yanaangalia umuhimu wa vyama vya siasa kubaki nguzo muhimu ya demokrasia nchini, kugawa viti vya ubunge kwa vyama kutokana na uwiano wa kura ambazo chama kimepata, kutafanya vyama kujimaarisha na kutoa sera bora zaidi na ushindani mkubwa.

“Kwa mapendekezo haya tutakuwa na asimilia 40 ya wabunge wote wanawake bila ya kujumlisha wabunge wanawake watakaochaguliwa kutoka katika mamlaka za serikali za mitaa moja kwa moja kama kina Gertrude Mongela, Beatrice Shelukindo, Zainab Gama na Jenista Mhagama, hivyo tunaweza kufikia asilimia 50 ya wabunge wanawake iwapo vyama vya siasa vitateua wagombea 24 tu kati ya 124 wa mamlaka zilizopo sasa na kushinda,” alisema.

Alisema kwa mapendekezo hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitakuwa na kazi ya kugawa mipaka ya majimbo tena, bali mipaka itatokana na tangazo la rais la kutangaza mamlaka za serikali za mitaa.

“Mapendekezo haya yanaondoa nafasi ya rais kuteua wabunge, na badala yake Katiba ifanyiwe marekebisho ili rais aweze kuteua baraza la mawaziri nje ya wabunge ili wadhibitishwe na Bunge,” alisema.

Katika hali hiyo, Zitto alisema: “Ndugu Rais nakuomba uiagize serikali yako kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na kuitisha mjadala mpana wa kitaifa kupitia asasi kama vile RIDET ili kupata maoni ya Watanzania wengi zaidi na hivyo kuboresha demokrasia,” alisema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alipoulizwa kama ofisi yake imepokea barua hiyo, hakukubali wala kukataa.

“Ndugu yangu sijui kama barua hiyo imefika au la, nakuomba uwasiliane na Katibu wa Bunge, anaweza kukupa maelezo zaidi kama ombi lake litakuwa limewekwa kwenye Order Paper au unaweza ‘kumkoti Zitto mwenyewe,”’ alisema Rweyemamu.

Nakala ya barua hiyo imesambazwa kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Katiba na Sheria na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents