Habari

Zitto Kabwe kuhusu sakata la Bombardier ‘Serikali lazima ihojiwe’

Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Mhe Zitto Kabwe amekinzana na kauli iliyotolewa na serikali ikishutumu vyama vya upinzani kushiriki na kutoa taarifa za ndege kuzuiliwa nchini Canada, na kusema kuwa vyama vya upinzani vina wajibu wa kuihoji serikali.

Tokeo la picha la zitto kabwe
Mhe Zitto Kabwe

Zitto Kabwe amesema suala kama hilo ni lazima watu wahoji, na sio kama hawapendi maendeleo yanayofanywa na uongozi wa Rais Magufuli, isipokuwa wanataka serikali ifanye vitu kwa uhakika zaidi, ili kuepusha kujiingiza kwenye hasara na migogoro kama hiyo iliyojitokeza.

Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe na iwe tayari kutoa majibu, Sisi kama vyama vilivyo Nje ya Serikali Ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote, Pia ni haki yetu kupata Taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali. Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa. Majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo. Hili ni suala la kisheria na suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele”,ameandika Zitto Kabwe kwenye ukurasa wake wa Facebook huku akisistiza kuwa Serikali isichukulie suala hili kama la kishabiki.

“Suala la Ndege yetu kuzuiwa Canada lisifanywe Ni suala la ushabiki Kama ushabiki wa mpira. Ni suala la Nchi hili na mjadala wake uwe na hadhi hiyo. Kitendo cha Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa Kwa jambo la kisheria Kama hili ni utoto. Hakuna mwanasiasa anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi. Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi Sana ‘ My Country, Right or Wrong ‘. Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha Ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali Kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda”,ameandika Zitto Kabwe.

Hata hivyo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali ijitokeze mara moja itoe taarifa ya kuekeweka kuhusu kuzuiliwa kwa ndege hizo aina ya Bombardier .

“Hii ni nchi yetu sote. Hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwa pindwa. Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka Ndege kuzuiwa, iachane na tabia ya hovyo ya kutafuta mchawi ‘ kwamba eti wanasiasa Ndio wamesababisha ‘. Kutafuta mchawi ni kutowajibika Kwa maamuzi ya Serikali yenyewe”,ameandika Zitto Kabwe.

Taarifa hizo zimeibuka baada ya siku ya ijumaa ya tar 18 Agosti, Mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa CHADEMA Mh. Tundu Anthipas Lissu, kutoa taarifa kuwa ndege aina ya Bombardier mali ya ATCL imezuiliwa nchini Canada kutokana na deni ambalo serikali inadaiwa na kampuni ya ukandarasi.

SOMA ZAIDI: Serikali yamjibu Lissu kuhusu ujio wa Bombadier

Hata hivyo baada ya taarifa hizo serikali ilijibu kwa kuthibitisha uwepo wa suala hilo na kuongeza kuwa kuna ya watu  wa vyama vya upinzani wameshirikiana na makampuni ya nje kufungua kesi kama hizo, ili kuweka vikwazo kwa serikali kuweza kufanikisha mipango ya maendeleo inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.

By Godfrey Mgallah

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents