Habari

Zitto, Slaa wawa vigogo bungeni

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekutana Dar es Salaam kuchagua wenyeviti wa kamati mpya za Bunge ambapo wabunge machachari wa kambi ya upinzani na chama tawala, wameibuka washindi katika uenyekiti na unaibu wa kamati nyeti.

Na Joseph Lugendo

 

 

 

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekutana Dar es Salaam kuchagua wenyeviti wa kamati mpya za Bunge ambapo wabunge machachari wa kambi ya upinzani na chama tawala, wameibuka washindi katika uenyekiti na unaibu wa kamati nyeti.

 

 

 

Wabunge walioibuka na ushindi katika uchaguzi huo ulioonekana kutokuwa na shinikizo la vyama vya siasa ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA) ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Hesabu za Mashirika ya Umma na Makamu wake ni Mbunge wa Mbarali, Bibi Estherina Kilasi (CCM).

 

 

 

Wengine ni Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa (CHADEMA), ambaye tofauti na wagombea wa kamati nyingine ambao walikuwa na wapinzani, alipita bila kupingwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa huku Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai (CCM) akichaguliwa kuwa makamu wake.

 

 

 

Kwa upande wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo (UDP), amechaguliwa kuendelea na wadhifa wake wa uenyekiti ambapo Makamu wake alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kwamtipura, Bw. Zubeir Ali Maulid (CCM).

 

 

 

Aidha, Mbunge wa Same Mashariki, Bibi Anne Malecela (CCM), alichaguliwa kuongoza kamati mbili; Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambako alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Kamati ya Miundombinu kuwa Makamu Mwenyekiti.

 

 

 

Katika Kamati ya Haki na Maadili na Madaraka ya Bunge, Bibi Malecela atasaidiwa na Mbunge wa Mafia, Bw. Abdulkarim Shah (CCM).

 

 

 

Wenyeviti wengine waliochaguliwa katika kamati ni Mbunge wa Bumbuli, Bw. William Shelukindo (CCM), ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini akisaidiwa na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe.

 

 

 

Mbunge wa Handeni, Dkt. Abdallah Kigoda, alichaguliwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi akisaidiwa na Mbunge wa Morogoro Kusini, Bw. Hamza Mwenegoha (CCM).

 

 

 

Naye Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Muleba Kusini, Bw. Wilson Masilingi na Makamu wake ni Mbunge wa Ilala, Bw. Azzan Zungu.

 

 

 

Katika tukio lingine Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Lucy Owenya (CHADEMA) alilalamikia hatua ya kupangwa katika Kamati ya Viwanda na Biashara akiwa mpinzani peke yake huku kamati hiyo ikiwa na vigogo wengi kutoka chama tawala.

 

 

 

Mbunge huyo alitaja vigogo hao wa CCM ambao alidai kuwa watamzidi nguvu katika kamati hiyo kuwa ni Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Bw. Nazir Karamagi, Mbunge wa Makunduchi, Bw. Abdisalaam Issa Khatib, Mbunge wa Tanga, Bw. Bakari Mwapachu, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Bw. Joseph Mungai na Mbunge wa Rombo, Bw. Basil Mramba.

 

 

 

Bibi Owenya alisema atafikisha malalamiko hayo kwa Spika, Bw. Samwel Sitta, ili kamati hiyo iongezwe mbunge mwingine kutoka kambi ya upinzani watakayesaidiana naye.

 

 

 

Kamati ya Nishati na Madini chini ya Bw. Shelukindo na Dkt. Mwakyembe, inatarajiwa kuanza kazi leo Dar es Salaam kwa kusimamia semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Petroli na Umeme, ambayo ilivunjika wakati wa mkutano wa Bunge uliopita mjini Dodoma, baada ya wabunge kudai kupewa kwanza ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza kashfa ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents