
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) ilitoa taarifa mnamo Jumatatu, Julai 1, ikielezea masuala ya haki za binadamu yaliyozingatiwa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wenye utata katika muda wa wiki mbili zilizopita.
Ni watu wangapi walikufa katika maandamano ya Mswada wa Sheria ya Fedha 2024? KNCHR imeandika orodha ya masuala ya haki za binadamu wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024. Masuala hayo ni pamoja na,
“Uchunguzi wa maiti za waathiriwa bado haujafanywa. Waliofariki ni kutoka Nairobi (17), Nakuru (3), Laikipia (1), Narok (1), Kajiado (3), Uasin Gishu (4), Kakamega (1) , Kisumu (2), Kisii (1), Mombasa (3), Siaya (1), Kiambu (1), na Nandi (1) Tunawapa pole familia hizo,” taarifa hiyo ilisomeka kwa sehemu. Tume hiyo iliripoti kuwa visa 32 vya utekaji nyara na visa 627 vya ukamataji holela vimerekodiwa nchini humo.
Tume ya haki za binadamu pia ilibaini kushuhudia uharibifu wa mali za serikali kama vile Maktaba ya Kitaifa na majengo ya bunge. “Hali iliyoonekana ilikuwa “ya machafuko”. Tungependa kutoa wito kwa pande zote kujizuia. Wakati maandamano yanalindwa chini ya katiba, lazima yabaki ndani ya mipaka ya kisheria,” iliongeza. Mwishowe, KNCHR pia ilibaini kutumwa kwa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya kusaidia polisi, ikisema kwamba lazima izingatie vipengee vya kikatiba vinavyoheshimu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi.
21 waliuawa, 336 walijeruhiwa wakati wa maandamano Hapo iliripoti kuwa KNCHR ilikuwa imetoa ripoti ya kina kuhusu vifo wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024. Katika taarifa ya Jumatano, Juni 26, KNCHR ilikashifu Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji.
KNCHR ilidokeza kuwa uchunguzi wake ulionyesha kuwa utumiaji wa risasi za moto katika maeneo mbalimbali nchini uliwaua Wakenya 21. Tume ya haki za binadamu imeongeza kuwa waandamanaji 336 na maafisa wa polisi walipata majeraha mbalimbali wakati wa maandamano hayo.
cc. Tuko news
Imeandikwa na Mbanga B.