AfyaHabari

Afrika wanaongoza kwa kujiua- WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuzindua kampeni ya kuzuia kujiua barani Afrika, kufuatia kuwepo kwa ripoti nyingi za mauaji ya aina hiyo kutoka Afrika.

WHO inaitaja Afrika kuwa ndilo bara linaloongoza kwa watu wake kujiua zaidi duniani kuliko mabara mengine ambapo nchi sita kati ya 10 zinazoongoza kwa watu wake kujiua duniani zinatoka Afrika.

“Takriban watu 11 kati ya 100,000 hufa barani Afrika, ambayo ni zaidi ya wastani wa kimataifa wa kesi tisa za kujiua kati ya watu 100,000,” ofisi ya Kanda ya WHO Afrika imesema katika taarifa yao.

WHO imeongeza kuwa Afrika ina uhaba wa matabibu wa magonjwa ya afya ya akili ukilinganisha na dunia huku kati ya watu 5,000 anaweza kuwepo Mwanasaikolojia mmoja tu ikiwa ni chini ya mapendekezo ya WHO.

Akizungumza na TBCOnline, Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye pia ni Rais wa Chama Cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), Magolanga Shagembe amesema upo uhusiano mkubwa kati ya watu kujikatiza uhai na matatizo ya afya ya akili.

“Maumivu anayoyapitia [mtu] kutokana na tatizo alilonalo kwenye afya yake ya akili, hupunguza uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi. Mara nyingi wengi hujitoa uhai kwa sababu wanakuwa wamechoka kuishi na maumivu japo hii sio njia sahihi, njia sahihi ni kulikubali tatizo, kuwa muwazi na kutafuta msaada,” amesema Shagembe.

Shagembe ameongeza kuwa kukosekana kwa uelewa wa kutosha kuhusu afya ya akili huwafanya watu wengi waamini kuwa, kuwa na matatizo ya kisaikolojia ni ishara ya udhaifu, hivyo wengi hushindwa kuwa wawazi, hali ambayo huwafanya waishi kwa maumivu ya ndani huku wakijificha kwenye uso wa tabasamu la kuigiza.

Oktoba 10  ni Siku ya Afya ya Akili Duniani, mwaka huu WHO inalenga kutoa elimu kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na matatizo ya afya ya akili.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents