
Mwanaume ambaye jina lake halijawekwa wazi ameokolewa katika nyumba ya ghorofa mbili huko mjini Waterbury, Connecticut, New York Marekani alipofungiwa kama mateka ndani chumba na baba mzazi pamoja na mama wa kambo kwa miaka 20 tangu mwaka 2005.
Mwanaume mwenye miaka 32 hivi sasa mnamo Februari 17, 2025 alipatikana baada ya kuwasha moto chumba alichokuwa akiishi akifanya hivyo akiwa na mambo mawili kichwani kama sio kufa basi huenda angekuwa huru na kutoka nje kwa mara ya kwanza tangu akiwa na miaka 12.
Akizungumza akiwa kwenye gari la wagonjwa (ambulance) baada ya kuokolewa kutoka kwenye moto huo, mtu huyo ameeleza kuwa imepita mwaka mmoja tangu aliporuhusiwa kuoga hali iliyodhihirika kutokana harufu mbaya iliyokwepo kwenye gari hilo na kubainisha kuwa amekuwa mateka kwa kipindi hichi huku akifungiwa chumbani kwa takribani masaa 23 kwa siku.
Watu wa nje ya nyumba hiyo wamefichua kuwa mtu kwa mara ya mwisho kuonekana ni wakati alipokuwa shule ya Msingi ya Barnard huku mwalimu mkuu wa shule hiyo, Tom Pannone akidai kuwa mwaka 2005 baba yake mzazi Kregg Sullivan alimuondoa shuleni hapo ili asomeshwe akiwa nyumbani.
Hata hivyo kutokana hali ya mtoto huyo kuonekana kuwa dhaifu mwalimu huyo aliwasiliana na Polisi juu ya usalama wa mtoto huyo kwa kuwa akihisi mtoto huyo alikuwa akipata shida nyumbani ingawa Bw. Sullivan ambaye alifariki mwaka jana kwa wakati huo aliwalalamikia Polisi kuwa anasumbuliwa na tuhuma hizo ambazo hazikuwa na ushahidi.
Nyaraka za mahakama, zinaeleza kuwa kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 11 mtu huyo alifungiwa ndani ya chumba mchana kutwa na usiku na alipewa chakula na maji kidogo tu hali iliyopelekea kupata utapiamlo huku meno yake yakioza.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, mama yake wa kambo Kimberly Sullivan (57) alifikishwa katika Mahakama ya Juu ya Waterbury akishtakiwa kwa utekaji nyara, kushambulia, ukatili na kumfungia mtu kinyume cha sheria, mashtaka ambayo huenda yamemfanya kutumikia kifungo cha maisha yake yote gerezani ingawa alikana hatia mashtaka hayo.