Ahukumiwa miaka 30 jela kwa kukutwa na dawa za kulevya gramu 56
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Brandon Dashaurn kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia katika kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Mescaline zenye uzito wa gramu 56.04.
Shauli hilo la jinai namba 107/2023 hukumu yake hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Fahamu Kibona.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kibona amesema mahakama imezingatia maoni ya upande wa mashtaka kuhusu athari za dawa za kulevya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimataifa pamoja na utetezi wa mtuhumiwa na kwamba katika kuzingatia maoni hayo imetoa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 gerezani.
Hakimu Kibona amesema pamoja na adhabu hiyo mahakama inatoa amri kielelezo ambacho ni gramu 56.04 za dawa za kulevya aina ya Mrescalinre kiharibiwe kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya.
Aidha Hakimu Kibona amesema haki ya kukata rufaa ipo wazi.
Mshtakiwa Dashaurn alikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) nOVEMBA 12, 2022 huko maeneo ya Posta wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam akiwa anachukua kifurushi chenye dawa hizo ambazo akiziagiza kutoka nchini Peru.
Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa hyo alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Mescaline.
Awali Wakili wa Serikali, Titus Aron aliieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka unaomba kutolewa kwa adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa kwani madhara ya dawa za kulevya kama yalivyoelezwa katika taarifa ya mkemia kuwa yanasababisha ulevi usio ponyeka, kuharibikiwa na akili na kwamba dawa hizo zipo kwenye kundi la sumu.
Aron ameeleza dawa hizo zinaharibu akili ya vijana ambao ni nguvu kazi katika ukuaji wa uchumi katika jamii na kusisitiza kuwa athari zzake ni mbaya za zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu..
Hivyo Aron aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wale ambao wanafanya biashara hiyo ya dawa za kulevya au kwa wale wenye mpango wa kujiingiza kwenye biashara hiyo haramu.
Hata hivyo mtuhumiwa katika utetezi wake aliiambia mahakama kuwa dawa hizo alikuwa akitumia kama kiburudisho cha kuweza kumsaidia kurelax.
Aidha alipoulizwa juu ya maombi yake dhidi ya shatka linalomkabili, aliiambia mahakama kuwa ifanue inayoona inafaa katika kutoa adhabu yake.
Written by Janeth Jovin