Ajichoma moto kisa kunyimwa uraia, hawapati huduma za kijamii

Hamad, mwenye umri wa miaka 27, alijichoma moto nchini Kuwait mnamo mwezi Desemba kitendo kilichoshangaza wengi nchini humo.

Taifa hilo dogo lenye utajiri wa mafuta, halionekani kama lenye kusababisha mtu kufanya kitendo kama hicho. Lakini Hamad anatoka jamii ya Bidun isiyokuwa na uraia nchini Kuwait.

Bidun ni neno la kiarabu linalomaanisha kukosa uraia ambako kwa watu wa jamii hiyo kunamaanisha kuwekewa masharti hivyo basi wanakosa baadhi ya huduma za jamii kwasababu ya hadhi yao, yaani hawawezi kupata elimu, matibabu wala ajira. Na kwa bahati mbaya Hamad na familia yake wanatoka jamii hiyo.

‘Niliumia sana nikifikiria machungu ya kaka yangu’

Kilomita 17 kutoka mji wa Kuwait, Sulaibiya eneo lililo mbali na mjini.

Omar anaishi huko na wazazi wake na ndugu zake 10 na familia yao katika nyumba yenye vyumba vitano ambako raia wengi wa jamii ya Baidun wanaishi hivyo.

Omar, 33, ana uhusiano wa karibu sana na ndugu yake mdogo, Hamad.

“Ni kijana muungwana, mkimya ambaye kila wakati anatabasamu,” Omar anasema.

Lakini takriban mwaka mmoja uliopita kaka yake mdogo alikuwa akijitenga na kujifungua kwenye chumba na pia alikataa jaribio la kaka yake kumtoa ndani ya nyumba na kujaribu kuzungumza naye.

Omar anasema ‘niliumia sana nikifikiria machungu ya kaka yangu’

Suala la Bidun huko Kuwait ni la tangu mwaka 1961 wakati ambapo baadhi ya familia waliokuwa wanaishi katika mpaka wa nchi hiyo hawakutuma maombi ya kupewa uraia baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza.

Nchi zingine kama Kuwait zenye raia wasiokuwa na uraia

Mataifa mengine ya Uarabuni kama vile Saudi Arabia na UAE pia nazo zina raia wasiokuwa na uraia, ambao kizazi chao ni makabila ya kuhama hama ambao walikuwa wakiishi katika eneo hilo lakini wakashindwa kutuma maombi taifa hilo lilipopata uhuru wake.

Kwengineko katika eneo hilo wengine pia hawana uraia baada ya serikali kuwavua uraia wao kama vile Bahrain ambapo baadhi ya walioasi walipokonywa uraia.

Katika serikali ya Kuwait, tatizo hilo bado linakanganya ambako raia wa jamii ya Bidun wanatambuliwa kama “wakaazi haramu”.

Inasema kuwa watu 34,000 pekee kati ya zaidi ya 100,000 ya wasiokuwa na uraia nchini humo wanaweza kutuma maombi ya kupata vitambulisho vya taifa na kwamba wengine waliosalia ni wa asili wa nchi zingine au uzao wao.

Changamoto za kila siku

Baada ya Hamad kumaliza shule ya msingi, hakuweza kujisajili katika shule ya upili ya umma kwasababu yeye hadhi yake ni Bidun na familia yake haikuwa na uwezo wa kumsomesha katika shule ya kibinafsi.

Hamad as a child

Kijana huyo alikua akitazama baba yake na kaka zake wakipata kipato kidogo kupitia biashara ya kununua na kuuza magari: wangeuza gari moja mwezi mmoja na kuanza tena kutaabika kwa kipindi cha miezi minne.

Inaonekana moyoni mwake hayo hayakuwa maisha aliyoyakubali. Kaka zake wanasema ndoto yake ilikuwa ni kujiunga na jeshi.

Lakini kwasababu alikuwa na machaguo kidogo, Hamad alifanya kila aliloweza kuishi mara ya kwanza alianza kwa kuuza matikiti maji mitaani hadi pale askari wa mji huo walipomkamata.

Baadaye akajaribu kufuga njiwa ambao walikuwa wanauzwa kwa dola 1.65 lakini akaachana na kazi hiyo baada ya kuona kwamba anapata hasara.

Hamad alipomaliza kifungo chake cha miezi minane kwa kuiba kondoo na kuziuza, kaka yake mwingine, Jasem alimtafutia cheti cha usafiri na kumpeleka Morocco.

Omar anasema safari hiyo ambayo ilikuwa ni mapumziko ilimfanya kaka yake kuonja maisha mengine mapya.

“Aliona dunia, aliona maisha na alikuwa na furaha. Alikuwa huko kwa wiki tatu lakini ilikuwa ni kama ameishi nchi hiyo kwa miaka mitatu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata, alikuwa tu akizungumzia safari yake ya Morocco.”

Vifo vingi vya kujitoa uhai

Hivi karibuni, Hamadi alianza kumuambia mama yake kwamba alitaka kujiendeleza kimaisha, aoe na kuanza maisha mapya. Lakini kwasababu tayari familia hiyo inapitia changamoto za kifedha, mchango wake ulikuwa mdogo sana na hakukuwa na kingine zaidi ya kumkumbusha kila wakati kuwa “Mungu atawezesha”.

Omar anasema alikuwa amewahi kuzungumzia kujitoa uhai lakini familia yake haikutarajia kwamba anaweza kutenda anachosema hadi ilipofika asubuhi moja na kwasababu ya kukosa matumaini, akajichoma moto.

Kufuatilia tukio hilo, mbunge Marzouq al-Khalifah alitoa wito kwa serikali kuunda kamati itakayochunguza sababu ya vifo vingi vya kujitoa uhai ambavyo vmekuwa vikitokea katika jamii ya Bidun.

“Tunaishi kwa nchi yenye baraka… lakini bado kuna watu wanaojitoa uhai kwasababu ya maisha magumu wanayopitia kila siku.”

Marzouq al-Khalifah

Mwanaharakati wa Bidun Abdullah al-Rabah anasema angependa kuona raia 34,000 wa Bidun wakitambuliwa kama wanaostahili kupewa urai na wengine kupewa haki za kiraia ambako kutawawezesha kuishi maisha yao kama wengine.

Mwanaharakati huyo, 35, anaongeza kuwa yeye na wengine kama yeye wanahisi haja ya kuwa na uaminifu kwa nchi hiyo ambako ndiko walikozaliwa lakini pia anaelewa changamoto wanayopitia vijana wa jamii yake.

“Hiki ni kizazi cha tatu ambacho bado hakijapata ufumbuzi wa suala hilo, je watasubiri kwa muda gani? Bila shaka ni tatizo linalowaathiri.”

Kwa Omari, kile anachotaka sasa hivi ni kusaidia kaka zake kwa kila namna.

Majina yote katika taarifa hii yamebadilishwa kwasababu ya kuwalinda.

Related Articles

Back to top button
Close