Habari

Akamatwa kwa kuotesha miche ya bangi nyumbani kwake

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata mtu mmoja akiwa ameotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake kwa kutumia glasi za plastiki.

Hayo yamebainishwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo ambapo amesema kuwa mtu huyo amekatwa mkoani Arusha na bangi hizo huko nyumbani kwake.

Lyimo amesema kuwa katika mkoa Arusha jumla ya kilogramu 98.55 za bangi, kilogramu 162.111 za mirungi, gramu 301 za heroin na gramu 195 za dawa aina ya methadone, pembe moja ya ndovu na risasi 11 za moto vilikamatwa.

“Matokeo haya yanathibitisha kuwa uhalifu wa dawa za kulevya mara nyingi huambatana na uhalifu mwingine, ikiwemo biashara haramu ya silaha na ujangili wa wanyamapori. Pia kuwepo kwa ongezeko la uchakachuaji wa dawa za kulevya kwa kuchanganya kemikali na vitu vingine ili kuongeza wingi wa dawa hizo kunaongeza athari za kiafya kwa mtumiaji” amesisitiza Lyimo.

Kanda ya Ziwa, hususan wilaya ya Rorya Mara, hekari 24 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, huku watuhumiwa sita wakikamatwa. Kanda ya Pwani, inayojumuisha mikoa ya Mtwara, Pwani na Ruvuma, zilikamatwa kilogramu 322.201 za bangi, kete nane na misokoto 216 ya bangi. Pia ekari nne za mashamba ya bangi ziliharibiwa na watuhumiwa nane walikamatwa kususika. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hususan mkoa wa Mbeya kilogramu 21 za bangi zilikamatwa huku watuhumiwa 11 wakishikiliwa.

Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. “Kwa pamoja, tunaweza kulinda jamii yetu dhidi ya athari za dawa hizi hatari. Mamlaka inawahakikishia watanzania kuwa, tutaendelea kupambana na mitandao yote ya uhalifu wa dawa za kulevya kwa nguvu zote na kuhakikisha tunavunja mitandao hii katika maeneo yote nchini” amesisitiza Lyimo

Kamishna Jenerali Lyimo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa kuhusu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo, na yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Naye Fatina Ramadhani, afisa mtendaji wa kata ya Haubi, amekiri kuwa baadhi ya wananchi katika eneo hilo wanajihusisha na kilimo cha bangi na amewaomba waachane na kilimo hicho, kwani matumizi ya bangi husababisha madhara mengi kwa mtumiaji. Aidha, ameeleza mbinu wanazozitumia kama kata kutokomeza dawa za kulevya.

“Tunafanya mikutano ya kijamii ambayo hueleza bayana madhara ya dawa hizi. Pia tunafanya doria mbalimbali katika msitu huu kwa kushirikiana na polisi jamii, askari wa akiba na wahifadhi ambao ni TFS,” alisema Fatina.

Kwa upande mwingine, Mhifadhi wa Misitu, Amon Titus Mlimwa, akimwakilisha Meneja Wakala wa Huduma ya Misitu wilaya ya Kondoa, amewashukuru wakazi wa Haubi kwa kujitolea kufyeka bangi. “Misitu hii ni kwa faida yetu sisi wenyewe. Tutaendelea na doria kila siku kwani viongozi wa kijiji na kata ya Haubi wamekubali kutoa ushirikiano kuhakikisha tunalifanikisha hili,” alisema Mlimwa.

Mkazi wa Mafai Kata ya Haubi, Abushekhe Hamis Kalinga amethibitisha kuwa, baadhi ya vijana wanajihusisha na matumizi ya bangi.

“Vijana wengi walikuwa wameshaanza kuathirika, japo wengine wanadai wanalima bangi kwa ajili ya pesa lakini ukilinganisha hasara na faida, hasara ni kubwa zaidi kuliko faida. Tusipoangalia kizazi kijacho kitakuwa na watoto wasio na akili timamu.”

Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji juhudi za pamoja kwa serikali, jamii na vyombo vya usalama kushirikiana.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents