AL Ahly yaihofia Yanga
Kocha Mkuu wa Kikosi cha AL Ahly Marcel Koller amewataka wachezaji wa kikosi chake kuongeza umakini wakati watakapopambana na Yanga katika wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuhitimisha makundi utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Koller alisema “Mchezo huu ni muhimu kwa timu zote Katika harakati za kuwania kuongoza kundi ingawa kwa jinsi nilivyoiona mechi ya Yanga dhidi ya Belouizdad nimegundua nina kazi kubwa ya kufanya.”
“Walicheza vizuri mechi yao ya mwisho hivyo ni lazima tucheze kwa tahadhari kubwa ili tuweze kutoka na matokeo chanya kwenye mchezo huo, sitaki kuzungumzia mchezaji mmoja mmoja kwa sababu nilichokiona ni kuwa wako pamoja wakishambulia na kwenye kuzuia wakizuia” alisema Marcel Koller Kocha mkuu wa Klabu ya AL Ahly ya Misri.
Mchezo wa mwisho wa AL Ahly alioucheza kwenye Ligi aliibuka na ushindi wa magoli 5-1 dhidi ya Baladiyat El Mahalla na baadhi ya wachezaji wao muhimu waliweza kurejea baada ya kutoka kwenye majeraha.
Mchezo wa AL Ahly dhidi ya Yanga ni wa kukamilisha ratiba tu kutokana na timu zote kufuzu hatua ya robo fainali ingawa vita kubwa iliyopo ni nani wa kumaliza wakwanza kwenye kundi D mpaka sasa AL Ahly ameambulia pointi 9 huku Wananchi wakiwa na pointi 8.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipowakutanisha ulifanikiwa kuisha kwa sare ya 1-1 huku Mfungaji pekee kwa upande wa Wananchi akiwa ni Pacome Zouzoua na kwa upande wa mafarao wa Misri ni Percy Tau.
Mchezo wa mwisho unatarajiwa kupigwa kesho siku ya Ijumaa tarehe 1/3/2024 katika Uwanja wa Cairo International Stadium majira ya saa 1:00 Usiku.
Imeandikwa na Mbanga B.