Aliyebakwa na Baba yake mzazi afunguka mazito

Binti (14) kidato cha kwanza mkazi wa Msangalale, Dodoma, anayefahamika kwa jina la Niache Nisome (sio jina lake halisi), anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana usiku wa Jumapili Aprili 26, 2026, na baadaye kupatikana akiwa ametupwa kwenye korongo huku akiwa hana fahamu na kudaiwa kubakwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya binti huyo, anadai alibakwa na watu wanne akiwemo baba yake mzazi.
Inaelezwa kuwa siku ya tukio, majira ya usiku akiwa anatoka kunyoa akiwa na rafiki yake, gari jeusi lilisimama ghafla na watu waliokuwemo ndani yake kumlazimisha kuingia kabla ya kutokomea naye kusikojulikana.
Rafiki aliyekuwa naye alitoa taarifa nyumbani, na juhudi za kumtafuta zilianza mara moja bila mafanikio. Inadaiwa kuwa majira ya saa nne usiku, familia ilifika Kituo cha Polisi kutoa taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo.
Majirani wa eneo hilo wamedai kusikia taarifa za kupotea kwake usiku huo na kushiriki katika jitihada za kumtafuta.
Mama wa binti huyo, akiwa katika hali ya majonzi, amesema mtoto wake alimweleza kuwa aliwaona baadhi ya watu waliomshambulia, akiwemo baba yake mzazi ambaye alidai alimwambia:
“Kwanini unachukua chuki ya Mama yako?”
Mama huyo amesema hana mgogoro mkubwa na mzazi mwenzake isipokuwa changamoto za muda mrefu zinazohusiana na malezi ya mtoto huyo.
Kwa upande wake, baba anayehusishwa na tuhuma hizo amekanusha kuhusika.
Akizungumza na BongoFive, amesema madai hayo yanachochewa na mgogoro wa muda mrefu kati yake na mama wa mtoto huyo.
Aidha, amedai kuwa kwa muda mrefu aliwahi kuomba kufanyika kwa vipimo vya DNA ili kuthibitisha uhusiano wake na mtoto huyo lakini hakupata ushirikiano.
Mtuhumiwa huyo pia amesema kuwa siku ya tukio alikuwa Zanzibar kwa shughuli za kikazi na kisiasa, akieleza kuwa yeye ni kiongozi na mwanachama wa CCM.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha kupokea taarifa ya tukio hilo na kusema uchunguzi bado unaendelea.
Kama una tukio lolote la ukatili, mkasa wasiliana nasi kupitia 0716265838
Fuatilia mkasa mzima YouTube BongoFive




