Aliyekuwa RC Simiyu Nawanda alivyokana kulawiti na kuachiwa kwa dhamana

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza na kusomewa shitaka moja la kumwingilia kinyume na maumbile Tumsiime Ngemela (21) katika eneo la Rock City Mall jijini Mwanza.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika mahakama hiyo mapema jana Julai 9, 2024 na kusomewa shitaka hilo ambalo anadaiwa kulitenda Juni 2, 2024 katika eneo hilo kinyume na kifungu cha sheria cha 154 kifungu kidogo (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Erick Maley, Waendesha mashtaka wa serikali ambao ni Wakili Magreth Mwaseba na Martha Mtiti waliitaja kesi hiyo kuwa ni kesi namba 1883 ya mwaka 2024.
Baada ya kusoma shtaka hilo, Mwaseba aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kuisomewa hoja za awali.
Hatahivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo, Wakili Constanstine Mutalemwa ambaye anamwakilisha mshtakiwa huyo aliomba mteja wake apatiwe dhamana kwa sababu kosa analoshtakiwa linadhaminika kisheria.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbbili, Hakimu Maley alisema dhamana ipo wazi hivyo mshakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja akiwa mtumishi wa umma na mwingine kutoka sekta binafsi na bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Milioni tano.
Mshtakiwa huyo ametimiza masharti hayo ya dhamana na yupo nje.
Baada ya kukamilisha masharti hayo, Mshtakiwa yupo nje ya dhamana hadi Julai 16, 2024 ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa hoja za awali huku upande wa mlalamikaji ukitakiwa kwenda na mashahidi.
Written by Janeth Jovin