Baraza la Mawaziri la Donald Trump latishiwa Maisha
Wateule kadhaa wa baraza la mawaziri la Donald Trump na wateule wa timu yake ya White House wamekuwa wakilengwa kwa vitisho vya mabomu.
FBI inasema, inafahamu kuhusu “vitisho vya mabomu, kupitia simu za uwongo.” Vitisho hivyo vilitolewa kwa takribani watu tisa waliochaguliwa na Trump kuongoza Idara za Ulinzi, Makazi, Kilimo na Kazi, pamoja na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, miongoni mwa wengine.
Polisi wanachunguza matukio hayo yaliyotokea Jumanne usiku na Jumatano.
Karoline Leavitt, msemaji wa timu ya mpito ya Trump, anasema walioteuliwa na Trump “walilengwa kwa vitisho vya vurugu, juu ya maisha yao na wale wanaoishi nao.”
Si Leavitt wala FBI waliowatambua wahusika kwa majina hadi sasa.
Vyombo vya usalama vinasema, Trump, ambaye alinusurika majaribio mawili ya kuuawa wakati wa kampeni yake, hakuwa miongoni mwa waliopokea simu hizo za uongo.